Sunday, 10 November 2013

PINDA ASEMA UHABA WA CHAKULA WANUKIA BAADHI YA MIAKOA YA TANZANIA

 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema baadhi ya maeneo nchini yatakabiliwa na uhaba wa chakula.
Akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge la 10 Mkutano wa 13 mjini hapa jana, Pinda alisema halmashauri 61 zinatarajiwa kukumbwa na uhaba wa chakula.
Aliitaja mikoa ya halmashauri zitakazokabiliwa na uhaba huo kuwa ni Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora.

“Natoa wito kwa halmashauri zinazohusika katika mikoa hiyo kufuatilia kwa karibu utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa kutoka maeneo yenye ziada na kuhakikisha kuwa kinafika mapema kwenye maeneo yao kabla ya wananchi wa maeneo hayo hawajaanza kulalamika,” alisema.
Alisema serikali inaendelea na tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe katika halmashauri 61 kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.
\
“Nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahimiza wakulima hasa walioko katika maeneo yenye chakula cha ziada kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya kaya zao,” alisema Pinda.
Aliwataka Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula kujipanga vizuri kuhamisha chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka kwenye maeneo yenye hali tete ya uhaba wa chakula.
Hata hivyo, alisema pamoja na serikali kuhakikisha kuwa kuna chakula cha kutosha, serikali imepanga kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kununua tani 250,000 za nafaka katika msimu wa 2013/14.

Alisema hadi kufikia Oktoba 23, 2013, wakala alikuwa amekwishanunua kiasi cha tani 218,412 za nafaka sawa na asilimia 87.37 ya lengo lililowekwa ambapo tani 217,919 kati ya hizo ni za mahindi na tani 493 ni za mtama. Aidha, alisema hadi Oktoba 23, 2013, maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na jumla ya tani 232,921 za nafaka, kati ya hizo tani 232,419 ni za mahindi na tani 493,103 ni za mtama.
Akizungumzia umeme vijijini, Pinda alisema baada ya tathmini kufanyika, zabuni 15 za kupeleka umeme vijijini zilipata makandarasi.

Alisema mikoa ambayo ilipata makandarasi katika awamu hiyo ni pamoja na Arusha, Dodoma, Iringa, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora.
Aidha, alisema makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kupozea umeme vya msongo wa Kilovoti 11 na 33 vya Ngara, Kibondo, Kasulu, Kigoma, Tunduru na Mbinga walipatikana.
Alisema miradi hiyo inatarajia kukamilika Juni, 2015 ambapo jumla ya Sh. bilioni 430.82.

Alisema Mei, 2013 zabuni nyingine 10 za miradi yenye thamani ya Sh. Bilioni 450 zilitangazwa kwa ajili ya kuwapata wakandarasi kupeleka umeme vijijini katika mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa na Tanga.
Waziri Pinda aliahirisha Bunge hilo hadi Desemba 3, mwaka huu litakapokutana kama Bunge la Katiba katika Mkutano wa 14.
10th November 2013
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

0 comments: