Friday 18 March 2016

Rais Magufuli Anasa Wauza Madawa ya Kulevya 3,000 Kimyakimya.....


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema ikiwa ni miezi mitatu tu tangu aingie ofisini baada ya kuteuliwa Desemba 10, mwaka jana na kuapishwa siku mbili baadaye, mpaka sasa tayari watu 3,000 wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Kauli hiyo ya Waziri Kitwanga inakuja ikiwa ni siku chache tangu Ofisi ya Hazina inayoshughulikia udhibiti wa mali za nje ya Marekani (Ofac), kutangaza kushikilia mali za raia wa Tanzania, Ali Khatib Haji Hassan maarufu kama ‘Shkuba’, zilizo nchi mbalimbali, kutokana na kumtuhumu kuwa ndiye msambazaji mkubwa wa dawa hizo kutoka Afghanistan kwenda barani Asia, Marekani na eneo kubwa la Afrika.

Wakati Marekani ambayo pia imepeleka suala hilo kwenye Bunge la Congress tangu ilipotoa taarifa hiyo, Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (International Narcotic Control Board – ICBC), nayo ilitoa ripoti ya mwaka 2015 iliyolenga Afrika na Tanzania, ikionyesha kuwa Tanzania ni kichochoro cha kupitisha dawa za kulevya zinazosambazwa karibu nusu ya dunia.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, Kitwanga alisema:

“Kama utakumbuka mara tu nilivyoteuliwa, nilisema suala la dawa za kulevya tutapambana nalo na siogopi kufa, nilisema na narudia tena siogopi kufa, hili ni suala la kufa au kopona.

“Hatutakubali tena Tanzania iingize dawa za kuleva au iwe njia ya kupitishia kwenda sehemu nyingine, au hata kama soko, kikubwa tunachokifanya sasa ni kujenga mifumo itakayozuia kabisa dawa kuingia nchini kwetu na zile zilizopo zitafutwe na zikamatwe, ndiyo sababu tunasema tumekamata watu wengi sana kwa muda mfupi sana ili kuhakikisha dawa za kulevya hazipitishwi hapa Tanzania.”

Alipoulizwa idadi ya watu waliokamatwa, Kitwanga alisema: “Kwa muda niliokaa hapa, zaidi ya watu 3,000 wamekamatwa, kuna wakubwa sana, wakubwa wa kati, wale wanaopokea tumewakamata zaidi ya 20, wanaosambaza tumekamata zaidi ya 100 na wale wanaouza kidogo kidogo ndiyo wengi zaidi." na kuongeza:

“Lakini bado tunaendelea na sasa hivi siyo suala tu la kwamba tukukamate na dawa za kulevya, tunakwenda mbali zaidi kwamba ukitajwa au tukikuhisi, tuone na utuhakikishie kwamba wewe kweli siyo muuza dawa za kulevya.

“Kuhisiwa tu ni kwamba lazima tufanye uchunguzi wetu utuhakikishie kuwa wewe siyo muuza dawa za kulevya.”

Akizungumzia mkanganyiko wa kauli aliyonukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa ana orodha ya majina ya wauza dawa za kulevya, Kitwanga alisema alinukuliwa vibaya.

“Watu walininukuu vibaya, ile ya kwamba nayajua (majina ya wauza dawa), huwezi ukawajua wote, hata ukijua, utajua kidogo tu, kinachotakiwa ni kuweka mfumo wa kufumua kila kitu, na huo ndiyo tumeuweka na tunaendelea kuuimarisha,” alisema na kuongeza:

“Nilisema jamani mimi sijapewa orodha, na siijui orodha, mimi ninachotaka kutengeneza ni kujenga mfumo utakaohakikisha kwamba dawa za kulevya haziingii na zilizopo ndani zinakamatwa na wahusika wote wanakamatwa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”

Alipoulizwa kama alipoingia ofisini alikuta orodha ya  wauza dawa za kulevya na majangili ambayo kiongozi mmoja wa serikali ya awamu ya nne alisema anayo, Kitwanga alisema yeye haangalii orodha, kazi yake ni kuwasaka wauza dawa hizo tu.

“Mimi nadhani sikumbuki sana, lakini nakwambia sasa hivi, sisi siyo suala la orodha, sisi ni suala la kuwasaka, kuwakamata na tutaendelea na hii siyo ya siku moja, siyo ya siku mbili ni endelevu, niwapo wizarani mimi, nisiwapo wizarani, kwa sababu tunajenga mfumo,” alifafanua Kitwanga.

Alisema kazi yake ni kujenga mfumo utakaohakikisha dawa za kulevya haziingia nchini na kwamba mfumo uliokuwapo awali ulikuwa dhaifu kidogo.

0 comments: