Sunday 20 March 2016

Azam FC yaipiga Bidvest 4-3, sasa kukipiga na Esperance


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imeidhihirishia tena umwamba Bidvest Wits ya Afrika Kusini baada ya kuichapa mabao 4-3 kwenye mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika uliomalizika jioni hii ndani ya Uwanja wa Azam Complex.
Ushindi huo umeifanya Azam FC kusonga mbele hadi raundi ya pili ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 7-3 ikiwa ni baada ya kuichapa timu hiyo mabao 3-0 ugenini wikiendi iliyopita jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Benchi la Ufundi la Azam FC liliingia kwenye mchezo kwa kufanya mabadiliko ya mchezaji mmoja tu kutoka kwenye kikosi kilichoshinda ugenini, akiingia Kipre Tchetche kuchukua nafasi ya Didier Kavumbagu aliyeanza na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ jijini Johannesburg.
Mabadiliko hayo yameongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji siku ya leo baada ya Tchetche kuibuka shujaa akifunga mabao matatu peke yake yaani hat-trick huku akiiweka katika wakati mgumu safu ya ulinzi ya Bidvest muda wote wa mchezo huo, ambao ulichezwa katika jua kali lililowasumbua wachezaji wote.
Bidvest iliuanza kwa kasi mchezo huo ikitaka kupata bao la uongozi, lakini bao lililofungwa na Tchetche dakika ya 22 kwa kichwa akimalizia krosi ya Ramadhan Singano ‘Messi’ liliwaondoa mchezoni, kabla ya kupigwa la pili dakika ya 42 na nahodha Bocco aliyemalizia vema pasi ya straika huyo hatari wa Ivory Coast.
Wageni hao walijipatia bao la kwanza dakika moja baadaye likifungwa na Pule Maliele kabla ya mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Gait Metodious Oting kwenda mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kuanza kwa kasi na Tchetche aliendeleza wembe wake wa kupachika mabao baada ya kutupia bao la tatu dakika ya 56 baada ya kupokea pasi safi ya Sure Boy na kumlamba chenga kipa wa Bidvest Barr Jethren kabla ya kutupia mpira wavuni.
Bidvest ilijipatia bao la pili dakika ya mbili baadaye lililofungwa na Mosiatlhaga Koiekantse akimalizia pasi ya Botes Henrico kabla ya Tchetche kukamilisha hat-trick yake dakika ya 88 kwa kuipatia Azam FC bao la tatu kwa kumchambua kipa wa wasauzi hao.
Baada ya kuingia bao hilo Tchetche alishindwa kuendelea a mchezo huo baada ya kupata maumivu ya enka huku Azam FC ikiwa imemaliza nafasi zote tatu za wachezaji wa akiba na hivyo kufanya wacheze dakika tatu za mwisho wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja.
Wakati mpira huo ukielekea kumalizika, Henrico alifanikiwa kuipatia Azam FC bao la tatu Bidvest kwa kichwa na kufanya mpira huo kuisha kwa wao kupigwa mabao 4-3.
Hivyo Azam FC imekata tiketi ya kucheza na Esperance de Tunis ya Tunisia kwenya raundi ya pili mchezo wa kwanza ukifanyika jijii Dar es Salaam Aprili 10, mwaka huu huku wa marudiano ukipigwa wiki moja baadaye.
Esperance imevuka hatua hiyo baada ya kuichapa Renaissance ya Chad jumla ya mabao 7-0, ikishinda 2-0 ugenini na jana ikaichapa 5-0 jijini Tunis.
Kikosi cha Azam FC:
Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Serge Wawa, Kipre Bolou/Farid Mussa dk75, Ramadhani Singano ‘Messi’, Himid Mao/Jean Mugiraneza dk 59, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco/Allan Wanga dk 78, Kipre Tchetche.

0 comments: