Saturday 13 December 2014

DENI LA TANESCO LAFIKIA .SH695.30 BILIONI NDANI YA MIAKA MINNE TU

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi98uPhH6eetjrYnRtJJpaMbCQNcetOWN2Wf4seRkPIfG0fVYZBUe4conMn0Q3ptM90BigYNVbfeZTZUc2mFLZwRLeWa1OxW4LuxQv9OqKKCM1rXI2xwYuF0vFBpzmbUQS85a4SNwhxtpA/s1600/CIMG3759.JPG


Makao makuu ya Tanesco jijini Dar es Salaam. 

DENI la Shirika la Umeme (Tanesco) katika miaka minne iliyopita, lilifikia kiwango cha juu cha Sh bilioni 695.30 mwishoni mwa mwaka jana.

Taarifa za uhakika zilizofikia gazeti hili wiki hii, zimebainisha kuwa ukuaji wa deni hilo, ulisababishwa na hali ya ukame uliolikumba taifa kuanzia miaka ya 2011.

Kutokana na hali hiyo iliyokosesha Tanesco umeme wa bei rahisi kutoka katika vyanzo vya maji, shirika hilo kwa mujibu wa taarifa hiyo, lililazimika kununua umeme ghali kutoka kwa wazalishaji wa umeme binafsi, ikiwemo mitambo ya kukodi ya dharura.

Ukuaji, ufutaji

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwaka 2011 deni la Tanesco lilikuwa Sh bilioni 538.47 ambapo ilipofika mwaka 2012, deni hilo lilipaa na kufikia Sh bilioni 563. Mwaka 2013 deni hilo ndio lilikuwa kubwa zaidi na kufikia Sh bilioni 695.30.

Hata hivyo mafanikio ya ufanisi wa Tanesco katika miaka ya hivi karibuni, yamesaidia kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuri na kufikia kiwango cha asilimia 97, ambapo fedha iliyopatikana ilianza kutumika kupanua huduma ya umeme nchini, kuendesha Shirika na kulipa madeni inayodaiwa.

Kutokana na mafanikio hayo kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanesco iliweka mkakati maalumu wa kuwalipa wadeni wake wakubwa kiasi cha Sh bilioni tatu kwa wiki, kwa kila mdai na kusaidia kushusha deni hilo kutoka Sh bilioni 695.30 mwishoni mwa mwaka jana, mpaka Sh bilioni 355,11 mwezi huu.

“Ukweli ni kwamba deni la Tanesco limeshuka kwa kiasi kikubwa… hivyo ni matarajio ya Shirika kumaliza deni hilo mwaka kesho,” ilieleza taarifa hiyo.

Kukatika kwa umeme

Taarifa hiyo pia imebainisha kuwa kukatika katika kwa umeme nchini, kunasababishwa na kuzeeka kwa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme.

“Ikumbukwe kuwa, kwa kipindi cha karibu miaka kumi Tanesco iliwekwa chini ya PSRC (Kamati ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma) kwa nia ya kubinafsishwa mwaka 1997 – 2007. “Katika kipindi hiki, Tanesco haikuruhusiwa kuwekeza wala kufanya ukarabati wa miundombinu yake, hivyo hali hiyo ilisababisha kuchakaa kwa miundombinu hiyo, ikiwemo mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme.

“Hata hivyo baada ya Serikali kubadili mtazamo wake wa kubinafsisha shirika, mipango kabambe ya kufanya ukarabati wa miundombinu hiyo na kujenga mipya, inaendelea ili kuwa na mfumo wa usafirishaji na usambazaji umeme ulio wa uhakika,” ilieleza taarifa hiyo.

Wakati kazi hiyo ikiendelea, taarifa hiyo imeeleza kuwa Tanesco ilishaelekezwa kutoa taarifa kwa umma kuhusu katizo lolote la umeme, lililopangwa kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya umeme na imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vyombo vya habari vikiwemo televisheni, radio, magazeti na magari ya kufikisha taarifa kwa maeneo yanayoathirika.

Utetezi wa ufanisi

Katika hatua nyingine, baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Tabora wameungana na Watanzania wengine nchini kumuomba Rais Jakaya Kikwete, kutumia busara na hekima katika kuamua kuhusu wanaotuhumiwa kuhusika na sakata la utoaji wa Sh bilioni 182.77 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT).

Wananchi hao wakiwemo viongozi wa kisiasa, dini, wafanyabiashara na wakulima wamesema pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Bunge katika kushughulikia sakata hilo, lakini kuna dalili za utashi wa kisiasa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, ambaye pia ni Shekhe, Said Ntahondi aliomba Rais Kikwete atumie busara zaidi kwa kumwajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, kwani kuna mengi ya maslahi ya taifa anayoendelea kutekeleza.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega, Amos Kanuda alishauri Rais afanye uchunguzi wa kina na kuzingatia kuwa Profesa Muhongo amefanya mengi kwa ajili ya maslahi ya Watanzania na manufaa ya umma.

Naye Mohamedi Ndago, mkazi wa Kijiji cha Kilimahewa wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara alisema anaona kuwa Profesa Muhongo, aliingizwa katika sakata hilo kwa hila na ushabiki kutokana na uchangiaji wa wabunge ulioegemea zaidi katika vyama wakati suala la Escrow lilipojadiliwa bungeni.

“Hapa tulipo ndio makao makuu ya wilaya hii, lakini kwa kipindi kirefu tumekuwa hatuna umeme...ila chini ya utendaji na usimamizi wa Muhongo, leo tuna umeme na baadhi ya vijiji pia vina umeme na maendeleo sasa yanaonekana...kitu cha kujiuliza hapa kwani kabla ya waziri huyo wizara haikuwepo? Mbona hutukupata umeme?” alihoji Ndago.

Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), Costantine Akitanda, jana aliitisha mkutano na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na kusema wananchi walitarajia kuona suala la akaunti ya Tegeta Escrow, likijadiliwa kwa kina na kuzingatia ukweli ili kupata ufumbuzi wa kudumu, lakini badala yake mjadala ulijikita kwa watu fulani na sio kujadili jambo husika.

‘’Hii maana yake ni kwamba lazima uchunguzi huru ufanyike kuweka bayana jambo hili, badala ya kuacha mambo yalivyojadiliwa kiujanja janja na kufanyiwa uamuzi kisiasa zaidi ndani ya bunge. “Pia naunga mkono kauli iliyotolewa na Ikulu kwamba utafanyika uchunguzi utakaobainisha uhusika wa baadhi ya watu wanaotajwa katika sakata hili,’’ alisisitiza.

Naye mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji, alihoji kauli iliyotolewa na Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, kuhusu fedha za Mfuko wa Changamoto ya Milenia (MCC) ambazo Tanzania ilitakiwa kupata kama msaada, kuonekana kumshinikiza Rais katika suala hilo la fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.

Alisema kauli hiyo haipaswi kuvumiliwa, kwani ni kama kumfundisha kazi Rais jambo ambalo si sawa.

“Alitakiwa akae kimya hakutakiwa kusema hayo maneno, sidhani kama Balozi wetu kule Marekani anaweza kumuelekeza Rais Obama namna ya kufanya kazi zake, ni jambo lisilowezekana,” alisema Dewji.
HABARILEO

0 comments: