Saturday 6 December 2014

P0LISI APIGWA NA WANANCHI BAADA YA KUKAMATWA NA MKE WA MTU

 


WAKAZI wawili wilayani Kahama, wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga baada ya kujeruhiwa katika mapigano kati yao na askari Polisi, baada ya kumshika ugoni mmoja wa askari katika hoteli moja maarufu mjini Kahama.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku baada ya mmoja wa vijana hao, kumkuta askari akijivinjari na mkewe, ndipo alipomshirikisha ndugu yake na kuibuka mapigano makali ya kurushiana makonde yaliyosababisha baadhi yao kujeruhiana vibaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, (PICHANI_alisema tukio hilo limetokea baada ya askari, Sajenti Edward kufumaniwa akiwa na mke wa mmoja wa vijana hao aliyejulikana kwa jina la Paschal Matonange (26).
Kamugisha, alisema baada ya kufumaniwa akiwa na mwanamke huyo chumbani, vijana hao walianza kumshushia kipigo huku wakimpiga picha akiwa uchi, hali iliyosababisha vurugu kwenye hoteli hiyo iliyopo nje kidogo na mji wa Kahama.
Kamanda huyo, alisema baada ya vurugu hizo wasamalia wema walijaa eneo hilo na baadhi yao kupiga simu kituo cha polisi ambako askari walifika kujaribu kutuliza vurugu hizo bila mafanikio.
Alisema katika kutuliza ghasia hizo, yalizuka mapigano makubwa kati ya vijana hao na askari polisi, hali iliyosababisha kujeruhiwa kwa baadhi ya askari na vijana hao ambao wamelazwa katika hospitali ya Halmashauri ya Mji.
Aidha, waliolazwa ni pamoja Marco Matonange (27), na mdogo wake Paschal Matonange ambaye ndie mme wa mwanamke huyo aliyefumaniwa akiwa na askari.
Hata hivyo, Kamugisha alisema jeshi lake litamchukulia hatua za kinidhamu askari aliyefumaniwa na mke wa mtu, ambaye pia yumo kwenye kikosi maalumu cha kufanya uchunguzi wa makosa ya jinai, kwa kuwa kufanya hivyo ni utovu wa nidhamu.
“Kimsingi sisi kama polisi hatuhusiki na masuala ya ugoni na askari kwenda pale kwenye tukio hawakwenda kwa ajili ya kufumania, bali walikwenda kwa ajili ya kutuliza ghasia lakini ilikuwa ni kazi kuwakamata hao vijana, mpaka sasa pamoja na wao kujeruhiwa pia baadhi ya askari wamejeruhiwa,” alisema Kamugisha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, alisema suala hilo  kwa kutumia nafasi yake ya uenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, analifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.
“Ni kweli tukio hilo ninalo, vyombo vyangu vya usalama vinalifanyia kazi ikiwemo uchunguzi ili kujua hasa chanzo chake kilichosababisha kuwepo kwa mapigano hayo,” alisema Mpesya ingawa mmoja wa majeruhi hao alidai mkuu huyo ndie aliyewaokoa wakati wakipata kipigo kituo cha polisi baada ya kupiga simu kwa mkuu wa polisi Wilaya (OCD).
Akizungumzia tukio hilo katika Hospitali ya Mji wa Kahama, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, aliyefika kuwapa pole majeruhi, alisema jeshi la polisi linatakiwa kufanya kazi kwa misingi ya sheria.
Mgeja, alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP), Ernest Mangu, kuhakikisha anafanya uchambuzi wa askari wake wasiokuwa na nidhamu ambao hutekeleza majukumu yao kwa vitisho, hali inayosababisha wananchi kukosa imani nao.
Mganga mkuu wa Hospitali ya Mji wa Kahama, Deogratius Nyaga, alisema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri.
Chanzo-mwanafalsafa blog

0 comments: