Saturday 13 December 2014

MUGU WANGU MGAWO WA ESCROW WAENDELEA KUMCHANGANYA PROF TIBAIJUKA.

 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Prof. Anna Tibaijuka. akiwa na waziri mkuu mizengo peter pinda
Juhudi za Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, kujisafisha dhidi ya kashfa ya kunufaika na mgao wa zaidi ya Sh. bilioni 300 zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, zimechukua sura mpya na sasa anaitumia shule ya wasichana ya Barbro Johansso, bodi yake, wanafunzi na wazazi kujinasua.

Prof. Tibaijuka ambaye aligawiwa Sh. bilioni 1.6 katika fedha hizo, tangu juzi ulianza mkakati wa kutoa matangazo katika magazeti na jana uliitishwa mkutano wa waandishi wa habari na Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Barbro Johansso Girls’ Education Trust (Joha Trust) inayomiliki shule hiyo, na ajenda kubwa ni kumtetea Prof. Tibaijuka.

Tibaijuka ni kiongozi wa waanzilishi wa shirika hilo, ambalo linamiliki shule mbili za sekondari; moja ya Barbro iliyoko jijini Dar es Salaam na nyingine ya Kajumulo Girls’ High School, iliyoko Manispaa ya Bukoba,mkoani Kagera.

Katika kumtetea, bodi hiyo imemuomba Rais Jakaya Kikwete kuona jinsi shinikizo la kutaka Waziri Tibaijuka awajibishwe serikalini linavyowachanganya na kuwakatisha tamaa wanaojitolea kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, hususan elimu.

Mkutano huo uliofanyika katika moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salam, uliwashirikisha wazazi, walimu, wahitimu, bodi ya shule pamoja na waandishi wa habari na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi, Salmon Odunga na Mlezi, Balozi Paul Rupia, pamoja na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Barbro, Halima Kamote.

Akitoa taarifa ya bodi hiyo kuhusu mgawo wa Sh. bilioni 1.6 aliopata Tibaijuka, Odunga alisema ulikuwa ni mchango alioupokea kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira, kwa ajili ya kuunga mkono shughuli zinazofanywa na shirika hilo.

Rugemalira ni mmoja kati ya watuhumiwa waliotajwa na Bunge kuhusika katika kashfa hiyo.

Odunga alisema hatua ya Tibaijuka mbali ya kuwa ni mwanzilishi, pia ni mtafuta fedha wa Joha Trust na kwamba, alipokea fedha hizo kutoka kwa Rugamalira ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Shirika la Misaada la Sweden (Sida), ambaye ni mfadhili mkubwa wa shirika hilo.

Alisema Sida ikihitimisha ufadhili wake kwa Joha Trust wa miaka 10 (2002-2012), ilihimiza bodi kuhamasisha michango ya ndani ili kujenga uendelevu na kukamilisha ujenzi wa mpango mkuu wa shirika hilo. 

“Kwa kuzingatia ushauri huo wa Sida, mwaka 2012 bodi ilimtaka mwanzilishi (Perofesa Tibaijuka) ambaye ni mtafuta fedha wa Joha Trust kuwaomba baadhi ya wafanyabiashara mashuhuri nchini kuunga mkono shughuli za asasi yetu kwa michango,” alisema Odunga.

Aliongeza: “Bwana na Bibi James Rugemalira ni miongoni mwa wafanyabiashara walioombwa mchango huo kwa barua ya tarehe 4 Aprili 2012 kupitia kampuni yao ya Mabibo Beer Wines and Spirits Limited.”

Alisema Februari, mwaka huu, bila kutaja ni kiasi gani, Rugemalira alimjulisha Tibaijuka kwamba, yuko tayari kutekeleza mchango ulioombwa na kumwagiza kwamba, sharti yeye afungue akaunti katika Benki ya Mkombozi ili kuupokea, kuufikisha shuleni na kuhakikisha unatumika kama ilivyokusudiwa.

Odunga alisema Rugemalira alieleza kuwa hakutaka kuhangaika kuhamisha fedha kwenda benki nyingine na kwamba, tayari kulikuwa na akaunti za shule.

Alisema Tibaijuka alifungua akaunti katika benki hiyo Februari 3 na kupokea fedha hizo kwa niaba ya shule Februari 12, mwaka huu kutoka VIP.

Odunga alisema bodi ilikaa kikao maalumu Februari 13 kupokea taarifa ya mchango huo kutoka kwa Rugemalira na kuukubali na kuamua utumike kulipa sehemu ya deni la shule ilizochukua kutoka Benki M.

“Kwa hiyo, mwanzilishi aliagizwa na bodi kuhamisha fedha hizo kutoka akaunti yake ya Mkombozi kwenda akaunti ya Benki M kulipia mkopo huo. Hii inafafanua kwa nini fedha zilihama kwa haraka kutoka Benki ya Mkombozi kwenda Benki M kwa wale wanaohoji suala hili,” alisema Odunga.

Alisema ili kutekeleza mpango mkuu, Julai 2011, Joha Trust ilikuwa imechukua mkopo wa Sh. bilioni mbili Benki M kwa ajili ya ujenzi wa bweni kubwa lenye uwezo wa vitanda 163.

Odunga alisema hadi kufikia Aprili 19, mkopo huo ulipolipwa wote, deni hilo lilikuwa limezaa riba na gharama nyingine na kuongezeka hadi kufikia zaidi ya Sh. bilioni 2.7.

“Kwa hiyo, pamoja na ukubwa wa mchango wa Rugemalira bado umelipia sehemu ya deni hilo tu. Sehemu nyingine iliyobaki (Sh. 1,124,274,444) imelipwa kutoka vyanzo vingine vya mapato ikiwamo mkopo wa milioni 291,374,444 zilizotolewa na mwanzilishi kulipa riba ya kila mwezi wakati wa uhai wa mkopo huo,” alisema Odunga.

Aliongeza: “Ilikuwa maamuzi ya bodi kupunguza madai hayo ya mwanzilishi kutoka takriban Sh. milioni 291 na kubaki takriban Sh. milioni 174. Kwa hiyo fedha zote alizozitoa Rugemalira za Sh. 1.617,100,000 zilitumika kulipa mkopo na wala hazikutosha. Katika hali hiyo, hisia na madai yanayotolewa kwamba mwanzilishi alijinufaisha na fedha hizo si kweli. Isingewezekana.”

Alisema shirika halina utaratibu wa kuwahoji wafadhili wao wa ndani au nje kwanza kuthibitisha chanzo cha fedha zao wanazowachangisha na kwamba, michango, iwe mikubwa au midogo, yote imekuwa ikipokelewa kwa nia njema wakiamini pia inatolewa kwa nia njema. 

Hivyo, alisema kwa kuwa walihakikishiwa na Benki ya Mkombozi kwamba, fedha za Rugemalira zilikuwa zimelipiwa kodi, walipokea mchango kwa furaha bila wasiwasi wowote. 

Alisema walishuhudia Bunge zima lilivyoazimia kwamba vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake kuhusu waliopata mgawo ili kuondoa mashaka na taarifa kamili zipatikane ili pale penye makosa hatua stahiki zichukuliwe.

Hivyo, akasema katika kikao cha bodi kilichoitishwa rasmi Desemba 2 kujadili jambo hilo, kwa kauli moja wanatamka kwamba, hawaamini kabisa na wanashindwa kuelewa kwanini Tibaijuka atakiwe kuwajibishwa nafasi yake serikalini kwa kuwa tu alipokea mchango wa shule kwa niaba yao.

“Jambo hili linatuchanganya na kutukatisha tamaa sisi wananchi wa kawaida tunaojitolea kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo hususan elimu. Tunaamini hatua hiyo pia itafifisha juhudi za viongozi wengine wengi wanaohangaika kuhamasisha michango ya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo elimu, afya, maji, vijana, walemavu, watoto yatima, watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi, wazee, wajane katika taifa letu change,” alisema Odunga.

Aliongeza: “Tunaomba mheshimiwa Rais alione jambo hili. Ikiwa michango ya maendeleo inayopokelewa na viongozi kwa niaba ya wadau wao itatafsiriwa kama zawadi zao binafsi kuna utata katika suala hili ili umma na viongozi wa ngazi za juu wapate ukweli juu ya jambo hili na ushiriki wetu.”

Baada ya kueleza hayo, ulizuka mvutano mkubwa kati ya waandishi wa habari na meza kuu baada ya kuonekana wahitimu na wazazi wakipewa nafasi zaidi ya kumsifu na kumtetea Tibaijuka na kutoa nafasi finyu kwa waandishi kuuliza maswali.

Baadhi ya wahitimu walimsifu Waziri Tibaijuka kwamba, amewasaidia kupata elimu bure na kuungwa na baadhi ya wazazi.

Hata hivyo, baadhi ya waandishi wa habari waliieleza meza kuu kuwa hoja iliyokuwa mezani wakati huo ilihusu kutaka ufafanuzi kama Tibaijuka kupata mgawo katika fedha hizo kulikuwa na nia ovu au la na kwamba, hakukuwa na tatizo katika wema na hisani iliyofanywa na waziri huyo pamoja na ubora wa shule zinazoendesha na shirika hilo.

Waandishi wengine waliieleza meza kuu sababu za kufanya haraka kutoa ufafanuzi huo wakati vyombo vya uchunguzi kuhusiana na kashfa hiyo vikiendelea na uchunguzi na kuhoji kama bodi haina imani na vyombo hivyo na itafanya ikiwa matokeo ya uchunguzi yataeleza kinyume cha ufafanuzi walioutoa. 

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Barbra ya jijini Dar es Salaam, Kamote alisema bado zinahitajika Sh. bilioni 12.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi majengo mbalimbali, ikiwamo klabu za wanafunzi, nyumba za wafanyakazi, msikiti, kanisa na ukuta wa kuzunguka shule.

Mlezi wa shirika hilo, Balozi Rupia alisema shule imekumbwa na wimbi la kadhia nzito, kwani mara zote mafahari wawili wanapopigana, nyasi ndizo zinazoumia.

Hata hivyo, alisema katika hatua waliyofikia, hakuna anayeweza kuzuia shule kuendelea na kwamba, mwenye nia ya kuiua, yeye ndiye atakayeanza kufa.

Aliwataka wazazi kutokufa moyo na yote yanayosemwa, kwani taratibu za kuwashughulikia watuhumiwa wote wanaohusishwa na kashfa hiyo, akiwamo Tibaijuka zipo na kwamba, walishtuka walipoanza kusikia kuwa baadhi ya wazazi wameshaanza kuwaondoa watoto wao shuleni kufuatia taarifa za kashfa hiyo.

“Wasweden watasikitika sana kuona tumesitisha kwa sababu ya Sh bilioni 1.6. Kutokana na uchunguzi unaoendelea kufanywa, tuko tayari kukaangwa…Najua kuna baadhi wanataka kuwa wabunge, marais ndyo tunawachanganya wazazi. Wenye makosa ndiyo watakaopata matatizo baada ya uchunguzi. Tuviache vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake,” alisema Balozi Rupia. 


CHANZO: NIPASHE 

0 comments: