Wednesday 3 September 2014

Tume: Polisi wanawatesa, kuwadhalilisha watuhumiwa

019

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema Jeshi la Polisi limekuwa likitumia nguvu kubwa katika kuwashughulikia watuhumiwa wa kesi mbalimbali nchini.
Pia imesema nguvu, ambayo imekuwa ikitumika kuwashughulikia watuhumiwa ni pamoja na kuwatesa, kuwadhalilisha, kuwabambikia kesi, kuwekwa kuzuizini kwa muda mrefu, bila kufikishwa mahakamani pamoja na mazingira magumu ya dhamana jambo linalokiuka haki za binadamu.
Imesema vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na polisi wakati wa kufanya mahojiano na watuhumiwa kwa kuwashinikiza kukiri makosa na kusababisha kuwa na idadi kubwa ya mahabusu na wafungwa na kuisababishia mzigo mkubwa serikali.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria wa Ttume hiyo, Nabol Assey, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema tafiti zilizofanywa na tume hiyo kwa nyakati tofauti hivi karibuni, zinaonyesha kuwa pia yamekuwapo malalamiko kutoka kwa watuhumiwa na wafungwa wanaolalamikia kubambikizwa kesi na polisi.
“Mara nyingi ukamataji unaofanywa na vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi mara nyingi, unakiuka haki za binadamu. Tafiti zinaonyesha kwamba, kumekuwapo na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa, ambayo huambatana na vitendo vya utesaji wa watuhumiwa, ambao unafanywa wakati wa mahojiano kwa lengo la kuwashinikiza kukiri makosa,” alisema Assey.
Aliongeza: “Hii inatokana na kukosekana kwa weledi kutoka kwa polisi wenyewe na uelewa mdogo wa sheria, kanuni na utaratibu zinazohusiana na haki za binadamu katika mfumo wa haki jinai.”

CHANZO: NIPASHE
Na Elizabeth Zaya
3rd September 2014

0 comments: