Friday 19 September 2014

WAANDISHI HABARI WANUSURIKA KUFA MKOANI KILIMANJARO


Waandishi wa Habari watatu mkoani Kilimanjaro wanusurika kifo katika matukio mawili tofauti ya kugongana na pikipiki wakiwahi katika majukumu yao ya kazi akiwemo Mwenyekiti wa Vijana wa CCM wilaya ya Hai.

Tukio hilo lilitokea asubuhi ya Jumatano majira ya 4:30 adhuhuri katika eneo la Kindoroko (Double Road) na maeneo ya Exim Bank mjini Moshi.

Waandishi hao wamefahamika kuwa ni Dixon Busagaga (Tanzania Daima na Clouds FM), Jackline Massawe (Radio Free Africa) na Arnold Jonathan (HabariLeo).

Arnold Jonathan anaelezea tukio hilo akiwa katika Hospitali ya St. Joseph ya mjini humo
“Asubuhi ya Jumatano, nilikuwa nikitoka nyumbani ninakoishi maeneo ya Njoro kuelekea katika kikao cha ndani chha kamati ya siasa kwenye ofisi za UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, nikiwa nimepanda bodaboda na dereva alipoigonga gari aina ya Noah iliyokuwa mbele yetu na mimi kurushwa na kuangukia juu ya gari hilo” .

Hali ya mwanahabari huyo na dereva wake inaendelea vizuri kwa sasa ingawa anadai kuwa kifua chake hakiko sawa.

Katika tukio la pili lililowahusisha wanahabari Dixon Busagaga na Jackline Massawe ambao wamelazwa katika Hospitali mbili tofauti ambazo ni KCMC na St. Joseph huku hali zao zikianza kuimarika kutokana na majeruhi waliyoyapata.

Dixon Busagaga anaelezea tukio jinsi lilivyowakuta
“ tulikuwa tumepakiza na mwenzangu (Jackline) tukielekea Moshi Golf Club kwa ajili ya majukumu ya kikazi ndipo tulipofika katika eneo la Moshi-Arusha wakati tukilipisha gari mojawapo lililokuwa likichepuka kuelekea upande tuliopo nndipo dereva wa bodaboda alipotuvaa kwa ghafla na kujikuta tupo katika hali hii”.

Dixon ameumia katika upande wa kulia ambapo sikio lake la kulia lipo katika hali mbaya pamoja na mkono wa kushoto, wakati Jackline ameumia maeneo ya kiunoni na goti la mguu wa kulia.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha bodaboda mkoa Kilimanjaro (CWBK) Bahati Nyakiraria alisema madereva wengi hawana udereva wa kujihami kama ambavyo sheria inawaagiza kufanya hivyo.

Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kuwataka madereva wa vyombo vya usafiri kuwa makini wanapokuwepo  barabarani.

: chanzo na JAIZMELALEO

0 comments: