Sunday 3 August 2014

LIGI KUU MIEZI MINNE YA MSIMU, HAKUNA MASHINDANO MENGINE YOYOTE HUYO MCHEZAJI FITI ATATOKEA WAPI?


LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, msimu wa 2014/2015 inatarajiwa kuanza Septemba 20 mwaka huu, na ratiba itatolewa mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo.
Yaani tutarajie wakati wowote kuanzia Agosti 20 ratiba ya msimu mpya wa Ligi Kuu itatoka.
Hiyo itafuatia kukamilika kwa zoezi la usajili, hatua ya kwanza ikikamilika Agosti 17 mwaka huu ikifuatiwa na kipindi cha uhamisho kitakachokamilika Agosti 17 mwaka huu wakati pingamizi itakuwa kati ya Agosti 19 hadi 26 mwaka huu. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itathibitisha usajili kati ya Septemba 1 na 2 mwaka huu.

Zoezi la uhamisho wa kimataifa, usajili wa wachezaji huru, na utatuzi wa dosari za usajili litafuatia ambalo linatakiwa liwe limekamilika hadi Septemba 7 mwaka huu kabla ya uthibitisho wa hatua ya mwisho ya usajili kufanywa Septemba 15 mwaka huu.
Tangu Juni mwaka huu klabu zimekuwa zikisajili na hadi Septemba 15 zoezi hilo litakapokamilika rasmi, itakuwa ni miezi mitatu.
Hata Ligi Kuu isingechelewa na ikaanza mwishoni mwa Mei kama kawaida, bado zoezi la usajili lingechukua si chini ya miezi miwili.
Lakini kwa kawaida, kwa misimu iliyotangulia, Ligi Kuu imekuwa ikianza mwishoni mwa Agosti au Septemba mwanzoni, na kumalizika Novemba.
Maana yake mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu unachezwa kwa miezi miwili au mitatu- tumemaliza kazi.
Baada ya hapo wachezaji wanakwenda kupumzika hadi watakaporejea kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, mwishoni mwa Januari au mwanzoni mwa Februari.
Na kutoka hapo watacheza mzunguko huo wa pili wa Ligi Kuu ya timu 14 hadi mwishoni mwa Aprili au mapema Mei, ligi inakuwa imemalizika na bingwa amekwishapatikana, timu za kushuka Daraja zimekwishajulikana.
Siri kubwa ya kufanikiwa kumaliza ligi haraka ni kuikimbiza, kuichezesha haraka kila wiki, kila timu inacheza wastani wa mechi mbili au tatu.
Pamoja na miundombinu yetu mibovu, lakini timu itasafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine mara tatu ndani ya wiki moja.
Mfano Azam FC, mabingwa wa msimu uliopita, waliimalizia wiki Tanga katikati ya wiki wakacheza mara mbili Mlandizi na mwishoni mwa wiki wakacheza Mbeya.
Baada ha kumalizika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Azam wakiwa mabingwa, zaidi ya wachezaji waliokwenda timu ya taifa, Taifa Stars- wachezaji wengine wa klabu za ligi hiyo hawakupata mashindano mengine yoyote ya kushiriki hadi watakaporudi kwenye ligi mwezi ujao.
Unaweza ukajiuliza iko wapi faida ya kuikimbiza Ligi Kuu kwa kasi hiyo ikiwa hakuna mashindano mengine mbele? Kitaalamu, mchezaji anatakiwa kucheza sana ili kuwa fiti, lakini kwa mchezaji wa Tanzania anayecheza Ligi Kuu kwa miezi minne hadi sita ya msimu, unatarajia nini?
Ndiyo maana kila siku tunawamezea mate wachezaji wa nchi jirani kama Kenya naUganda, kwa sababu wanacheza Ligi ndefu na bado wana mashindano mengine kama Kombe la FA na kadhalika.
Sisi ukisikia mashindano mengine ni ya ujanja ujanja tu ya wiki mbili mbili kama Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar, sasa saa ngapi unategemea kumjenga mchezaji katika kiwango cha ushindani?
Hapo hapo unamsikia mtu mwingine anahoji, hivi kwa nini wachezaji wa Taifa Stars watoke Azam, Simba na Yanga pekee, hakuna timu nyingine?
Anasahau kwamba Azam, Simba na Yanga ndizo ambazo kwanza zinasajili wachezaji waliong’ara kutoka timu nyingine- na pili ndizo ambazo zinacheza mechi nyingi kidogo kuliko timu nyingine.
Kutoka timu hizo tatu ndipo hupatikana wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Kagame, Ligi ya Mabingwa Afrika hata Kombe la Shirikisho- sasa kwa vyovyote lazima mchezaji wa timu ya taifa atokane na timu hizo.
Naziona jitihada za rais mpya wa TFF, Jamal Emil Malinzi katika kuhakikisha analeta mabadiliko kwenye soka ya Tanzania na kwa hakika anaonyesha matumaini.
Najua ni mengi ambayo anayafanyia kazi kwa sasa, na hili la ligi ya miezi minne hadi sita ndani ya msimu, vyema akalitupia jicho nalo, je kwa mtaji huu tutampata wapi mchezaji fiti? Asanteni.  

0 comments: