Monday 19 May 2014

MBEYA CITY WAKWAMA KWENDA SUDAN KISA CECAFA HAIJATUMA TIKETI

KIKOSI cha timu ya Mbeya City cha jijini Mbeya jana kilishindwa kuondoka nchini kuelekea Sudan kushiriki mashindano ya Kombe na Nile Basin kutokana na tiketi za ndege kutokuwepo.
Mbeya City imepata nafasi ya kushiriki mashindano hayo baada ya Azam kuikacha michuano hiyo ikieleza kwamba kwa sasa wachezaji wake wako likizo.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, aliiambia BIN ZUBEIRY kuwa bado hawajajua kikosi chao kitasafiri lini.
Kimbe alisema wachezaji 20 wa timu hiyo watawasili jijini Dar es Salaam leo Jumatatu asubuhi wakisubiri tiketi za kuelekea Sudan.

“Tulikubaliana awali timu yetu iondoke nchini Jumapili ili tupate muda wa kuzoea hali ya hewa, ila hadi leo  (Jumapili jioni ) tiketi hazijatumwa, TFF inaendelea na mawasiliano na CECAFA", alisema Kimbe.
Aliongeza kuwa wameona ni bora waje Dar es Salaam kuendelea na mazoezi na kusubiria safari hiyo wakiwa jijini.
"Timu ilianza mazoezi mapema na huko tutaenda kushindana na kuonyesha uwezo wetu na changamoto kama ilivyokuwa katika ligi", Kimbe aliongeza.
Alisema pia maandalizi yao yatawapa wachezaji wao uzoefu wa kimataifa na kuahidi kwamba msimu ujao Mbeya City itakuwa moto zaidi.
Katika ligi ya Bara Mbeya City ilimaliza ikiwa ya tatu nyuma ya bingwa Azam na Yanga walioshika nafasi ya pili. 
 habari Na Samira Said, Dar es Salaam

0 comments: