Monday 19 May 2014

ATLETICO MABINGWA LAKINI KOMBE ‘WANYIMWA!’



>>DIEGO SIMEONE ASIFIA KIKOSI CHAKE!
SANCHEZ_AIFUNGIA_BAO_BARCAJANA huko Nou Camp, Atletico Madrid walitoka Sare 1-1 na Barcelona na kutwazwa kuwa Mabingwa wapya wa Spain kwa kushinda La Liga wakiwa Pointi 3 juu lakini mara baada ya Mechi hiyo kwisha Mabingwa hao hawakupewa Kombe lao.
Habari toka huko Spain zinadai kuwa Kombe hilo maarufu la Ubingwa halikutolewa kwa vile Mkuu wa Shirikisho la Soka la Spain, Angel Maria Villar, alikuwa safarini.
Hadi sasa haijulikani lini Atletico watapewa Kombe lao.
Wakati huo huo, Kocha wa Atletico, Diego Simeone, amekisifia Kikosi chake kwa kutwaa Ubingwa wao wa 10 wa Spain, ikiwa ni mara ya kwanza tangu walipotwaa Mwaka 1996 wakati yeye akiwa Mchezaji wa Timu hiyo, na kushika Nafasi ya 3 kwa kutwaa Ubingwa wa Spain mara nyingi wakiwa nyuma ya Real Madrid, mara 32, na Barcelona, mara 22.
Pia, ushindi wa Atletico Msimu huu umefuta Miaka 10 ya Real na Barca kupokezana Ubingwa kwani mara ya mwisho Timu nyingine kutwaa Ubingwa ilikuwa Valencia kwenye Msimu wa 2003/04.
Diego Simeone alisema: “Leo ni Siku muhimu mno katika Historia ya Klabu hii.”
Atletico walitwaa uongozi wa Ligi mwishoni mwa Mwezi Machi lakini Ligi ilipokaribia ukingoni walisuasua na kufungwa na Levante na kutoka Sare Nyumbani kwao dhidi ya Malaga na kuhatarisha nafasi yao.
Hata hivyo, Diego Simeone alisema hakuwa na wasiwasi na Kikosi chake.
Ametamka: “Sijawahi kufikiria kuwa hatuwezi kuwa Mabingwa. Kikosi hiki Siku zote hujibu mapigo. Hata changamoto ikiwa kubwa vipi, wao Siku zote wana ari kubwa kuishinda. Kuwa Mabingwa dhidi ya Barcelona ni hisia kubwa sana!”

 

0 comments: