Mkurugenzi wa Kitengo cha Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bw. Marcel Katemba akiongea na waandishi wa habari( Hawapo pichani)kuhusu juhudi zinazofanywa na serikali katika kuyajengea mazingira mazuri ya ufanyaji kazi Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) ili kuongeza ushiriki na kutoa mchango wao katika kuleta maendeleo katika jamii, Wakati wa Mkutano uliofanyika leo Jiijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo Bw. Erasto Ching’oro.
PICHA NA GEORGINA MISAMA
***********************************
Na Jovina Bujulu-MAELEZO
Serikali kupitia uratibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto imeendelea kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya ya jamii.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Marcel Katemba leo jijini Dar es Salaam.
Mercel alisema kuwa serikali inaendeleza jitihada za kuwezesha Mashirika hayo ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na.24 ya mwaka 2002 na marekebisho yake ya mwaka 2005.
“Sera hii ni mwongozo mkuu kwa Taifa katika masuala ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ikiwa na lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa Mashirika hayo kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na ushirikano” Alisema Marcel.
Marcel aliongeza kuwa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inaendelea kusimamia sekta ya mashirika hayo na kutoa ushauri kwa Waziri mwenye dhamana ya uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta hiyo.
Aidha Baraza la Taifa la NGO’s linaendelea kuratibu utekelezaji wa kanuni za maadili ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa lengo la kujitawala, kutandaa na kuboresha huduma zinazotolewa na mashirika hayo.
Akifafanua zaidi Marcel amesema ubia na ushirikiano baina ya Serikali na NGO’s umeimarika kutokana na matamko ya kisera na elimu inayotolewa kwa wadau mbalimbali wa mashirika yasiyo yakiserikali.
Pia Serikali imeendelea kutoa misamaha ya Kodi na ruzuku kwa Mashirika hayo ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Juhudi za serikali za kujenga mazingira wezeshi kwa NGO’s zimepanua wigo kwa wananchi kujumuika na kushiriki katika maendeleo ya jamii ambapo zaidi ya wananchi 35,000 ni wanachama wa mashirika hayo yaliyo zaidi ya 6679 kote nchini.
*SIMBA CHAWENE AWATAKA WATANZANIA KUACHWA KUFANYA MAANDAMANO YA KUPINGA MCHAKATO WA KATIBA
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Simba Chawene akichangia mada bungeni mjini Dodoma.
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. George Simba Chawene amesikitishwa na kauli zilizotolewa na baadhi ya Wajumbe walioko nje ya bunge hilo kuhusiana na uhalali wa bunge hilo lililoko Kisheria.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akichangia mada katika mjadala ndani ya bunge hilo huku akisisitiza kuwa huo ni upotoshwaji mkubwa na watu hao wanapaswa kuangaliwa kuhusu uzalendo wao.
Mhe. Chawene ameeleza kuwa inasikitisha zaidi hasa pale shutuma zinapoelekezwa kwa Mwenyekiti wa bunge hilo, Mhe. Samuel Sitta, kuwa bunge hilo sasa linaonekana ni mali ya Mwenyekiti wa bunge hilo wakati si kweli.
“Gazeti linachukua kurasa tatu hadi nne kuzungumzia habari Sitta king’ang’anizi, hivi hili bunge lipo kama liliitishwa na Sitta ama na Rais wa nchi?, hili bunge liko kisheria”, alisema Mhe. Chawene.
Aliongeza kuwa kwa niaba ya Watanzania wanafanya kazi ya bunge hilo kwa mujibu wa sheria huku akisisitiza kuwa wajumbe waliotoka nje ya bunge hilo wamevunja sheria na kwamba hawawezi kutafuta uhalali nje ya sheria.
“Wanamlazimisha Rais avunje bunge hili, Rais wa kufuata utawala bora anavunja kwa mamlaka yapi? Mamlaka ya Rais yako kwa mujibu wa sheria”, alisema Mhe. Chawene.
Aidha, ameeleza kuwa Sheria inayoendesha mchakato wa Katiba ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imetungwa kutoka katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye hatua tatu zikiwemo hatua ya kukusanya maoni ambayo Tume ya Warioba ilifanya kazi hiyo na kumaliza, hatua ya Pili ni bunge hilo kujadili kwa niaba ya wananchi wa Tanzania kwa uwakilishi uliopo ndani ya bunge hilo na hatua ya tatu ni wananchi kwenda kutunga Katiba.
“Sisi hapa tunatoa Katiba inayopendekezwa, inayofuata ni Watanzania kwenda kutunga Katiba kwa kutunga kwa kupiga kura ya kusema ndiyo au hapana yale tuliyoyajadili na kuletwa na Tume”, alisisitiza Mhe. Chawene.
Aidha, amewataka watanzania kuwaona watu hao kuwa ni watu wabaya na wasio na nia nzuri na nchi na kuepuka kuingia barabarani kufanya maandamano ya kuipinga Katiba hiyo.
Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
0 comments:
Post a Comment