Wednesday 3 September 2014

AMEUAWA KWA KUNYONGWA NA BABA YAKE MZAZI

Mganga Geofrey Kilingwa ‘Simbaiwe’ amuua mwanaye



MTOTO Regina Geofrey (miezi 14), ameuawa kwa kunyongwa na baba yake mzazi Geofrey Kilingwa ‘Simbaiwe’ (27), kwa madai alizaliwa akiwa ametanguliza makalio yake.
Baba wa binti huyo ambaye pia ni mganga wa kienyeji anayeishi kitongoji cha Mwikang’ombe, Kijiji cha Katuma, Mpanda, alitenda unyama huo kwa madai mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza  makalio ni mkosi na nuksi kubwa katika shughuli zake hizo za uganga wa kienyeji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa,  mzazi huyo  aliyetenda uhalifu huo Julai 20 mwaka huu ambako alikamatwa na Jeshi la Polisi Agosti 26 mwaka huu.
Inadaiwa kuwa, siku hiyo ya tukio, mtuhumiwa baada ya kumnyonga hadi kufa binti yake huyo, alimzika kwa siri katika  kibanda chake anachofanyia shughuli zake za uganga wa kienyeji.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda Kidavashari alidai kuwa, mtoto Regina alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao haukufahamika  kwa zaidi ya mwezi mmoja, ndipo Simbaiwe alipolazimika  kuanza kumuuguza kwa siri pasipo mkewe kufahamu, kwani alimdanganya amepelekwa kutibiwa na babu yake  huko Mwanza.
Inaelezwa kuwa, kibanda anachofanyia kazi zake za uganga kiko mbali na makazi yake, hivyo ilikuwa rahisi kumficha mtoto wake huyo kwa zaidi ya mwezi mzima akimtibu bila mkewe kufahamu.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, wakazi wa kitongoji cha Mwikan’gombe wakiongozwa na  Mwenyekiti wao, walimtilia shaka mtuhumiwa kutokana na tetesi zilizozagaa eneo hilo kuwa  mtoto Regina alikuwa ameuawa na baba yake mzazi na kuzikwa kwa siri.
Inadaiwa wakazi hao na Mwenyekiti wao, walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuhoji alipo binti yake ambako alipinga vikali,  lakini alipopekuliwa kibandani kwake, walibaini kuweko kwa tuta  dogo lililokuwa limechimbwa siku za karibuni.
Kidavashari, aliongeza kuwa wakazi hao waliamua kufukua tuta hilo na kukuta kichwa cha mtoto huyo ndipo wakaitaarifu polisi .
Mama ya marehemu, Maria Exavery (22), alidai kuwa hakuhusishwa wala kupewa taarifa kwamba binti yake huyo amekufa.
“Mie nilikuwa nafahamu kuwa, Regina yuko kwa babu yake Mwanza akitibiwa,” alisema Maria.
Naye Regina Kaboni (40), mkazi wa Isamilo Mwanza, ambaye alikuwa akitibiwa na mtuhumiwa, anadai kuwa alishirikishwa katika maziko ya binti huyo.
“Hata hivyo…nilistushwa sana kwa kitendo cha mtuhumiwa kumzika mwanaye bila ya kumshirikisha mkewe, nilipomuuliza alidai kuwa kwa mila ya kwao, mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza makalio, mama mzazi wa mtoto ni mwiko kushirikishwa katika maziko ya mtoto huyo,” alidai.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, watu wanne wakiwemo  wazazi  wa marehemu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi  kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani mara tu baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Wengine wanaoshikiliwa na Polisi ni Regina Kaboni ni Msolwa Jacob (29), mkazi wa kitongoji cha Mwikang’ombe.

0 comments: