Monday 19 May 2014

CCM YAPINGA ZIARA YA MADIWANI WA MANISPAA YA IRINGA MIKOA YA DAR ES SALAAM, LINDI NA MTWARA


Hassan Mtenga, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kimeingia katika vuta nikuvute na baraza la madiwani la halmashauri hiyo kikipinga ziara ya madiwani wake kufanya ziara ya mafunzo katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.

Katika kupinga ziara hiyo CCM imemuandikia barua Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba ikieleza sababu zake za kufanya hivyo; barua hiyo imefikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma.

Katibu wa CCM wa manispaa hiyo, Hassan Mtenga ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa alisema; “chama hakioni kama ziara hiyo inataja kwasasa.”

Mtenga alisema wananchi wa manispaa ya Iringa wanakabiliwa na kero nyingi ikiwemo ya ubovu wa miundombinu ya barabara zake zilizoharibiwa na mvua zilizopita za masika.

“Mamilioni ya fedha wanayotaka kuyatumia kwenye ziara hiyo yanaweza kusaidia kurekebisha miundombinu hiyo na mambo mengine muhimu kwa wananchi wa manispaa yetu,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Ishengoma ambaye kiutaraibu ndiye mwenye dhamana ya mwisho ya kukubali au kukataa ziara hiyo alisema ameanza kulishughulikia suala hilo.

“Nimekutana na Katibu wa CCM, Meya na Mkurugenzi wa Manispaa; katika ushauri wangu wa awali nimeelezea umuhimu wa ziara hiyo, hata hivyo nimeshauri ifanyike katika mkoa mmoja wa Dar es Salaam kama ikibidi,” alisema.

Alisema halmashauri hiyo inaweza kuokoa fedha nyingi kwa kuachana na ziara ya Lindi na Mtwara na kuzitumia fedha zitakazookolewa kwa shughuli zingine za maendeleo.

Awali Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi alisema wataupokea ushauri wowote utakaotolewa na mkuu wa mkoa kuhusiana na ziara hiyo.

“Tutasikia ushauri wa mkuu wa mkoa, lakini na wa chama pia kwasababu sote tunatekeleza Ilani ya CCM; tutaona suala hili limekaaje baada ya kufikishwa mezani na tutakuja na maamuzi ya mwisho,” alisema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Theresia Mahongo alisema bajeti kwa ajili ya ziara hiyo (hakutaja kiasi chake) ilipitishwa mwaka jana.

Alisema madiwani hao walitaka kwenda Lindi, Mtwara na Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayoweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya manispaa ya Iringa.

Alisema wakati ziara ya Lindi inalenga kujifunza mbinu mpya za kuhamasisha utalii, ile ya Mtwara inalenga kujifunza miradi ya ujenzi wa majengo bora na ya Ilala Dar es Salaam mbinu za ukusanyaji mapato.

Alisema kufanyika kwa ziara hiyo kutategemea maelekezo yatakayotolewa na Mkuu wa mkoa na meya wa manispaa hiyo kwa mujibu wa taratibu za kiutendaji.

Pamoja na ufafanuzi wa watendaji hao, madiwani wa manispaa hiyo wameganyika kuhusiana na ziara hiyo, huku wachache wakiunga mkono ushauri wa CCM na wengine wakitaka ifanyike.

Baadhi ya madiwani wa CCM ambao ni wengi katika baraza hilo (hawakutaka majina yao yatajwe) walisema wanaunga mkono uamuzi wa CCM wa kupinga ziara hiyo.

Mmoja wa madiwani  hao alisema pamoja na umuhimu wa ziara hiyo, fedha hizo zinaweza kufanya makubwa kwa maendeleo ya manispaa hiyo.

“Na tungependa kwa lolote litakalofanywa itangazwe wazi kwamba limetokana na fedha zilizokuwa zilipwe kwa madiwani; hiyo itatupa heshima kubwa na hasa kwa kuzingatia kwamba tunakaribia kufanya Uchaguzi Mkuu,” alisema.

Diwani mwingine alisema ziara hiyo haina maana sana kwao kwa kuzingatia kwamba wana muda mfupi kabla ya kuingia katika harakati za Uchaguzi Mkuu ujao.

“Tunaweza kwenda ziarani, lakini lini hicho tutakachojifunza tutahakikisha kinatekelezwa; sioni haja ya kwenda ziara hiyo,” alisema.

0 comments: