Thursday, 14 November 2013

LEMA ACHUKUA HATUA JUU YA PICHA CHAFU ZINAZOSAMBAZWA KWA KUMZALISHALI

veronica Mheta, HabariLeo, Arusha — MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amesikitishwa na picha chafu zinazomdhalilisha na familia yake, ambazo zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii na simu za mkononi, kwa alichodai ni lengo la kumchafua kisiasa na chama chake.

Akizungumza jana ofisini kwake mjini hapa, Lema alisema picha hizo zilitumwa Oktoba 29 kwenye simu ya mkewe, Neema na bahati mbaya mtoto wake akapokea na kuziona, akashituka na kumwonesha mama yake.

Neema alisema alipoona picha hizo kwa mara ya kwanza Oktoba 29, alishtuka sana na akiwa katika hali hiyo, alipigiwa simu

na mama yake mzazi akilia na kumsihi amwombe mumewe aachane na siasa, sababu zimefikia pabaya.

Alidai baada ya kuzishuhudia, mkewe alimtumia Mchungaji Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini), kwenye simu yake ili kumwonesha siasa chafu zinazofanywa Arusha.

“Lakini mimi ninachosikitika sana ni picha hizi kupelekwa hadi kwa wakwe zangu na mama yangu mzazi ambao wameniambia kama siasa inafikia hapa bora niiache,” alilalamika Lema.

Alisema baada ya kufikiria hatua za kufanya, alitoa nakala nyingi na kuzipeleka ofisi ya Bunge, ambako alimwonesha Spika Anne Makinda na Naibu Spika Job Ndugai ambao walisikitishwa na picha hizo na kuahidi kumsaka mhusika ili ashughulikiwe.

Aidha, alidai kuwapo namba za simu zinazotumiwa kumchafua pia, ambazo zinatuma ujumbe mchafu kwa viongozi wa dini na watu wengine na kisha kuzimwa, lakini wahusika wakipiga namba hizo simu zinaingia kwa Lema na kuulizwa juu ya ujumbe aliotuma.

“Yaani kwa siku naweza kupokea simu zaidi ya 200 za watu wakilalamika kuwatumia ujumbe wa matusi na kuniuliza kama nina akili timamu, lakini mimi nasema Mungu atashughulika na hawa watu, japo tumejaribu kama chama kufuatilia Airtel wakatujibu tuachane na hilo jambo tutakufa,” alisema Lema.

Alitaja namba hizo za simu kuwa ni 0787717733, 0684941134, 0752593773 na 0688913046 ambazo alidai zinatumiwa kumchafua.

Kuhusu kupeleka suala lake Polisi alisema hawezi kufanya hivyo, kwa sababu liko mikononi mwa ofisi ya Bunge ambayo ni taasisi kubwa na inalishughulikia kwa uzito wa kipekee.

“Picha hizi nasambaza katika mikutano yangu yote, watu waone siasa chafu za mkoa wa Arusha na wajue jinsi viongozi tunavyotoa maisha yetu,” alisema Lema.

Pia alitumia nafasi hiyo, kuomba wafuasi wa chama chake wasilipize kisasi kwa mtu yeyote, ila wamwachie Mungu lakini aliahidi kuzisambaza kwa wafuasi wake ili waone propaganda chafu dhidi yake.

Naye Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema wamesikitishwa na mchezo mchafu unaofanywa na aliodai ni wapinzani wao wakubwa wa kisiasa na kuomba Serikali kuonya vijana wanaotumiwa kutengeneza picha hizo ili wasiendelee. 
chanzo  veronica Mheta, HabariLeo, Arusha

0 comments: