Mbunge wa Kahama, James Lembeli juzi aliwafungulia milango wanasiasa wanaotaka kugombea ubunge katika jimbo lake akisema ni ruksa kwa mtu yeyote akitaka wafanye kampeni za maendeleo kwani ndicho kinachohitajika na wananchi.
Lembeli alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Bugomba A, Kata ya Ulewe wilayani Kahama mkoani Shinyanga alipokwenda kutimiza ahadi zake kwa wananchi.
Hata hivyo, Lembeli, hakukubali wala kukataa kwamba atagombea tena ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwakani licha ya kubanwa na wananchi wakimtaka aendelee kutetea kiti chake kwa kuwa bado wanamhitaji.
Alisema kwa utaratibu wa chama chake (CCM), muda wa kujitangaza haujafika na kwamba kinachomsumbua ni namna wananchi wake watakavyopata maendeleo zaidi naye kumaliza ahadi zake na Izile za lani ya uchaguzi ya CCM.
“Nimekuja kutimiza ahadi kusaidia ujenzi wa zahanati. Nahitaji pia kushirikiana nanyi kujenga nyumba ya mganga, zote tumalize kabla ya mwisho wa mwaka huu ili wananchi wapate huduma bora, ndipo nitapata usingizi kwa kuwa watakuwa salama,” alisema Lembeli na kuongeza:
“Siwezi kuwazuia wanaopita na kujitangaza, muhimu waambieni waache porojo, wasaidie maendeleo kwanza kwa kuwa maendeleo hayaangalii chama wala kabila.”
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kahama Mabara Mlolwa, alisema muda wa wanasiasa kupita na kutangaza nia zao haujafika hivyo watakaobainika kufanya hivyo watashughulikiwa na chama.
Na Habel Chidawali-Kahama
0 comments:
Post a Comment