MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro |
MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amekeme vikali watu wote wanaopotosha umuhimu wa mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) wakisema ni njia ya kuwaingia wakazi wilayani hapa katika mfumo wa Freemasons.
Kwa wilayani Kyela,kupitia CHF kila mkazi anapaswa kulipia kiasi cha shilingi 5000 ili aweze kupata huduma za afya bure kwa kipindi cha mwaka mzima.
Lakini tafsiri ya bima hiyo kwa baadhi ya wakazi wilayani hapa imekuwa ni kuhusisha kupata huduma na mtandao wa Freemasons wakisema haiwezekani watu wakapata tiba kwa kiasi kidogo cha fedha kama shilingi 5000 kwa mwaka mzima.
Uwepo wa upotoshaji huo,umekuwa ukitajwa kuwa chanzo cha baadhi ya wakazi kugoma kujiunga na CHF na kusababisha wilaya kuendelea kusuasua katika uhamasishaji wa mfuko huo huku pia hatua hiyo ikisababisha wakazi wilayani hapa kuendelea kutumia fedha nyingi kugharamia matibabu.
Hapo jana akiwa katika kikao cha barala maalumu la madiwani kilichokuwa kwaajili ya kupitia na kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Kandoro alikemea vikali upotoshaji huo.
Alisema iwapo wapo watu ambao hawahitaji kaya zao kujiunga na mfuko wa CHF basi wanapaswa wakae kimya na kuendelea kugharamia matibabu yao badala ya kuendeleza uvumi na kuipotosha jamii na kuisababishia kuami katika mambo yasiyo na msingi kwao.
“Kama umekosa hoja ya msingi na hutaki kujiunga na mfuko basi acha na ukae kimya.Usiendelee kupotosha umma ili ukufuate kwa kuujaza maneno ya uongo na yasiyo na tija katika maisha ya mwanadamu” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliagiza uongozi wa wilaya kuhakikisha unatoa maagizo kwa viongozi wa vijiji na kata kuendelea kutoa hamasa kwa jamii kujiunga na mfuko huo ili kupunguza gharama za matibabu.
Alitaka pia kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mtu yeyote atakaeendeleza maneno ya upotoshaji akihusisha huduma zitolewazo na CHF na mtandao wa Freemasons kwakuwa mtu huyo atakuwa haitakii mema jamii inayomzunguka.
Kandoro aliitaka jamii kutambua kuwa mpango wa kuanzisha kwa CHF ulilenga wananchi waweze kuwekeza katika afya kwa kujiwekea bima ili mara watakapopata matatizo ya kiafya waweze kupata huduma hata kama hawatakuwa na uwezo wa kugharamia kwa wakati huo.
Source: Joachim Nyambo, wa habarileo
0 comments:
Post a Comment