Wednesday, 6 November 2013

BARUA YA EMMA YA KUOMBA KUFANYA MTIHANI NA KAULI YA WAZIRI"HAKUNA MIMBA YA BAHATI MBAYA"


 
Picture
Barua ya Emma
KISA CHA EMMA ROBERTS NA SHERIA INAYOONGOZA ELIMU TANZANIA

Kupitia kipindi cha Wanawake Live kinachorushwa na EATV kila siku ya Jumanne saa tatu usiku, umma wa Watanzania walipata kufahamu kilichomkuta binti Emma Roberts.

Kwa kukumbusha tu, Emma ni binti aliyefukuzwa shule kutokana na ujauzito. Ujauzito wa Emma ulikuja baada ya kufanyiwa kitendo cha ukatili cha ubakwaji. Kwa mdomo wake mwenyewe, Emma ameelezea hali halisi na kusema kwamba hakupenda huo ndio uwe mustakabali wake wa maisha kwa kuwa alikuwa na ndoto nyingi sana katika maisha. Emma hakupenda 
kubakwa. Tukio hilo limemkosesha nafasi ya kupata haki yake ya msingi, elimu. Emma katika maelezo yake anasema elimu ndio ingemsaidia katika maisha yake yeye na mwanae. Akiwa na namba yake ya mtihani tayari kwa ajili ya kufanya mtihani wa kidato cha nne 2013, Emma alisubiria kwa hamu majibu ya ombi lake kwa Wizara ya Elimu imruhusu kufanya mtihani huo. Hata hivyo, Emma hakuweza tena kufanya mtihani kwa kuwa hakupewa ruhusa ya kufanya hivyo.

Kupitia Wanawake Live, Waziri wa Sheria na Katiba Mhe Mathias Chikawe amezungumza na kueleza sheria ikoje katika masuala kama haya, na kumalizia kuwa 'Hakuna mimba za bahati mbaya'. 
Picture
Waziri, Chikawe
Maswali ambayo wengi wanajiuliza ni pamoja na Je, sheria inayotumika kuongoza elimu nchini Tanzania, inawanufaisha wananchi au ni sheria iliyowekwa kukandamiza kikundi fulani cha watu? Je, Emma Roberts hakupaswa kupigania haki yake ya kupata elimu eti kwa sababu Mhe Waziri wa Sheria na Katiba amesema kwamba 'Hakuna mimba za bahati mbaya'?

Mara zote jamii imeshuhudia wasichana wadogo wakifukuzwa shule kutokana na tatizo la mimba, bila kutazama chanzo cha mwanafunzi huyo kupata hiyo mimba. Pia, wahusika wakuu wa mimba hizo (wanaume) wengi wamethibitika kuendelea kupeta tu mtaani bila kuchukuliwa hatua zozote ilhali msichana anakuwa ameshafukuzwa shule na kunyimwa haki yake ya kimsingi.

Muda umefika sasa wanawake kupigania haki zao dhidi ya sheria kandamizi ambazo zinawanyima fursa muhimu katika maisha. Pia, mawazo mgando kama ya Mhe. Chikawe eti 'hakuna mimba za bahati mbaya' ni kitu kinachopaswa kupigwa vita vikali.
 
habari hii kwa hisani ya wanawakelivetv.com
 
Picture
Emma na mwanaye na Joyce Kiria

Source: wavuti blog.

0 comments: