Lukuvi amchefua Mbowe
*Ashangazwa na kauli aliyotoa bungeni
*Mtupa bomu adaiwa kubebwa na Polisi
*Mtupa bomu adaiwa kubebwa na Polisi
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe (kushoto), akimfariji Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari, katika Hospitali ya Arusha Medical Lutheran
Center (ALMC)
alikolazwa baada ya kushambuliwa na watu wanaodhaniwa kuwa
makada wa CCM Makuyuni, Monduli, mkoani Arusha juzi.
Pamoja na kulaani tukio hilo, Lukuvi aliwahusisha wanasiasa ambao hakuwataja kwa majina kuwa wanahusika katika kufanya uchochezi na kuwajaza wananchi chuki.
Alisema kuwa polisi waliokuwapo katika mkutano wa Chadema baada ya
kurushwa kwa bomu, walitaka kumfuatilia mhusika, lakini walishindwa na
kuamua kujihami baada ya wananchi kuwanza kuwashambulia.
Mbowe akizungumza jana jijini Arusha, alisema kuwa chama chake
kinao ushahidi wa picha zinazoonyesha jinsi Polisi walivyoshiriki
kutekeleza amri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kuwa kutokana na kuibuka maneno ya kupotosha yanayotolewa
na viongozi wa serikali ili kuficha ukweli wa tukio hilo, watalazimika
kuanika mambo yote hadharani.
“Kama Waziri anatoa kauli za namna hii kuwa vyama vya siasa ndiyo
wahusika wa kuchochea wananchi, wakati ukweli unaonekana nimemshangaa
sana, na serikali inajua ukweli wa hili na hata wakificha tutaenda hata
nje kutafuta ukweli,” alisema.
Alisema kuwa tukio hilo ni la kupangwa na serikali kwa kuratibiwa
na Jeshi la Polisi, kwa sababu hata Spika wa Bunge, Anne Makinda, haja
mpigia simu kumpa pole kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa
kunusurika kuuawa pia kwa Watanzania waliouawa.
“Hii inaonyesha jinsi gani tukio hili limepangwa na tumefanyiwa
hivi, nchi nzima magari yetu yamevunjwa na kuharibiwa vibaya na hata
Mbunge wetu wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, amepigwa katika Jimbo
la Edward Lowassa na kundi la CCM,” alisema.
Mbowe alisema kuwa anashangazwa kuona Polisi wako mstari wa mbele
kuchunguza tukio hilo la mauaji wakati wao ni waratibu wa tukio hilo.
Alisema wapo watu waliofanikiwa kuwaona warushaji na walipokimbia
kuingia katika gari na kuwa walifuatiliwa na kuona wanashushwa Polisi
kwenye gari la Toyota Land Cruiser la rangi ya bluu, likisindikizwa na
gari la Land Rover.
“Katika gari aliloingia mhalifu, walikuwamo Polisi wawili hadi
walipofika kituoni Polisi na kumshusha aliyelipua bomu hilo,” alisema.
Alisema katika hali ya kawaida alitarajia shughuli za Bunge
zisimame kwa ajili ya msiba huo, lakini mambo yakawa tofauti na watu
walivyozoea.
“Lakini cha kushangaza Polisi wamekamata watu watatu wa Chadema na
wanawatesa ili waonyeshe picha za video walizochukua, wakati wao siyo
wahusika wala hawajui kitu, wanawaonea bure,” alisema.
Alisema kama hali ni hiyo ya umwagaji damu, ni bora mfumo wa vyama
vingi ufutwe umma ujue moja kuliko kuhadaa ulimwengu kuwa kuna vyama
vingi wakati ni kiini macho.
Mbowe alisema hata Nassari alipokuwa akipigwa, Lema alikuwa na
Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul
Chagonja, akampa simu asikilize ili atoe maagizo kwa Polisi Monduli
kumsaidia Mbunge huyo, lakini Chagonja aliweka simu pembeni na hakutaka
kuongea na simu hiyo.
Alisema kutokana na hali hiyo wao wataendelea na harakati zao za
kisiasa hata kama watauawa na kuwa wanaamini kuwa chama kitaendelea kwa
sababu chama siyo Lema wala Mbowe.
Kuhusu kauli ya Lukuvi kwamba siku ya tukio Polisi walisaidia kuwaokoa watu, alikataa na kusema kuwa hakuwapo
hata mmoja aliyemnyanyua mtu kumpeleka hospitalini, hivyo huo ni uongo.
“Majeruhi wengi walioko hospitalini wana majeraha ya bastola na
hata marehemu aliyefariki siku ya kwanza Ramadhani Juma aliuawa kwa
kupigwa risasi kifuani,” alisema.
IDADI YA VIFO YAONGEZEKA
Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia watatu, baada ya Amiri Ally (9) kufariki dunia jana akiwa kwenye hospitali ya Selian.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Selian, Dk. Paul Kisanga, alithibitisha
kuwa Amir alikutwa na mauti akiwa amelezwa katika wodi ya wagonjwa wenye
uangalizi maalum (ICU).
HALI YA NASSARI
Pia Mbowe alisema hali ya Nassari siyo nzuri kwa sababu bado
anahitaji vipimo zaidi na kwamba madaktari kutoka Hospitali ya
Muhimbili, Kitengo cha Mifupa (MOI) watakwenda kumfanyia uchunguzi zaidi
kwa kushirikiana na
madaktari wa hospitali hiyo.
Akizungumza kwa tabu, Nassari alisema kuwa alizingirwa na watu
zaidi ya 40 wakiwapo Wasomali watatu, waliokuwa wakimpiga kwa marungu na
kilichomwokoa ni bastola aliyokuwa nayo.
“Hawa watu walikuwa na nia ya kuniua kwa sababu walikuwa
wakinishambulia zaidi kifuani, chini ya shingo na kichwani kwa kunipiga
na marungu kama mwizi, nilipoona hali mbaya nikajitahidi kukimbilia
kwenye gari langu na kutoa bastola yangu wakakimbia,” alisema.
Nassari alisema kundi la watu waliomshambulia alibahatika kuwatambua watu wawili ambao ni wakazi wa Wilaya ya Arumeru.
WAWILI WAHAMISHIWA NAIROBI
Dk. Kisanga alisema wagonjwa wawili ambao ni Fatuma Jumanne na
Sharifa Jumanne walikimbizwa jijini Nairobi, Kenya kwa matibabu. Wote ni
wa familia moja.
KATIBU WA LEMA HOI
Aidha, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema,
Gabriel Lucas, hali yake imebadilika na yupo ICU na kufanya idadi ya
majeruhi walioko ICU kuwa wawili akiwamo Fahad Jamal (7).
MAJERUHI ASIMULIA
Mmoja wa majeruhi alioko hospitalini hapo, Abdallah Alila (39),
alisema ameumia vibaya mguuni baada ya kupigwa risasi na askari polisi
na mguu mwingine kudondokewa na vipande vya bomu.
“Mimi nilikuwa nyuma ya jukwaa kuu nikimtazama Mbowe, alipomaliza
kutoa hutuba akashuka jukwaani na kukusanya sadaka, ndipo nilipoona
mfuko wa rambo mweusi mdogo unapeperuka juu, tukadhani upepo
unapeperusha, ghafla ulipotua tukasikia kishindo na akasika mama mmoja
apiga kelele kuwa aliyerusha anakimbia yule, nilipogeuka nikajikuta
nimenguka chini,” alisema.
“Lakini mwisho wa yote kijana aliyerusha hilo fuko aliingia katika
gari la Polisi na kuondoka mahali hapo kwa kasi, mimi nilikuwa chini
wakati huo naangalia kila upande,” alisema.
Alisema alikuwa ameangukia katika mtaro na watu waofika kutaka kumuokoa, aliwambia waondoke wajiokoe mwenyewe.
POLISI WATUPIWA LAWAMA
Baba mzazi wa marehemu Ramadhani Juma aliyeuawa katika ugaidi huo,
Juma Ramadhani, alisema kuwa anashangazwa kuona jopo la askari
wapelelezi wakifika nyumbani kwake Mianzini na kumtaka kukubali kutoa
mwili wa mtoto wake bila uchunguzi ili usafirishwe kwenda kwao Tabora
kwa mazishi.
“Hawa watu nashangaa wanadai kuna magari yapo manne kuwa
nitapelekwa nyumbani, lakini nimekataa kwa sababu wanadai nisikubali
Chadema kuhusika katika msiba huu, mimi sikubaliani nao kwa kuwa Mbowe
alinisaidia mwanzo wa tukio hadi mwisho alipofariki mikononi mwake,”
alisema.
Alisema hawezi kumwacha Mbowe kwa kuwa ni msimamizi wake katika hatua zote.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, jana hakupatikana kuzungumzia madai hayo.
Kila alipopigiwa simu ya mkononi hakuipokea.
SERIKALI YATANGAZA BINGO
Serikali imetangaza bingo ya Sh. milioni 100 kama zawadi kwa watu
au mtu atakayefanikisha kunaswa kwa mhalifu wa matukio ya ulipuaji
mabomu na mtandao wake.
Akifafanua Lukuvi alisema mtu atakayefanikisha hilo atapewa Sh.
milioni 10 fedha ambazo zitaendelea kutolewa kwa kila mtu na kama
zitakuwa zimemalizika basi serikali itatenga fedha nyingine.
DK: BILALI: WAHUSIKA WATAKAMATWA
Serikali imesema kuwa itafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa
waliohusika katika tukio la ulipuaji wa bomu hilo watatiwa mbarano na
kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alipowatembelea waathirika.
Alisema kuwa serikali imepokea kwa masikitiko makubwa tukio hilo
ambalo ni la kigaidi na kwamba haitasita kumchukulia hatua kali za
kisheria mtu yeyote aliyehusika na tukio hilo iwapo atakamatwa.
Aliwataka wananchi wavute subira, wawe wastamilivu na wavumilivu hususani katika kipindi hichi ambacho upelelezi unaendelea.
“Napenda kuwaambia msikate tama, vuteni subira kwani aliyehusika
atakamatwa tu hata kama ikitumia muda wa siku tatu, siku kumi mwezi na
hata miaka mitatu na zaidi lakini aliyefanya tukio hili atakamatwa tu
hata akienda wapi, ninachopenda kuwaambia wananchi kuwa mjenge imani na
serikali yenu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mshirikiane a mwishowe matatizo haya yatakwisha,” alisema Dk. Bilal.
MAREKANI YALAANI
Marekani kupitia ubalozi wake nchini, imelaani vikali tukio hilo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Balozi wa Marekani
nchini, Alfonso Lenhardt, alisema Marekani imelaani vikali tukio hilo la
kusikitisha na kwamba inatoa salamu za pole kwa familia zilizopotelewa
na ndugu zao na majeruhi kwenye tukio hilo la kusikitisha.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, tukio hilo la juzi linafuatia lile
lililotokea Mei 5, mwaka huu katika Kanisa la Katoliki la Mtakatifu
Joseph, jijini humo ambalo liliua watu watatu na kujeruhi zaidi ya 60.
Serikali ya Marekani imetoa wito wa kukamatwa, kushitakiwa na kisha
kuhukumiwa kwa wote waliohusika na tukio hilo la kusikitisha.
Alisema Tanzania ni nchi ambayo inajulikana toka zamani kwa utajiri
iliyonao wa utamaduni, uvumilivu na tofauti mblimbali lakini vitendo
kama hivyo vinataka kuitia doa, kutishia amani na usalama wa nchi hii
iliyojaliwa kuwa na ardhi kubwa.
Alfonso aliongeza kuwa, Marekani inasimama kama rafiki wa karibu
kwa Watanzana wote na kuwataka kupinga vitendo hivyo vinavyofanwya na
baadhi ya watu wanaojaribu kutishia usalama wao.
Pia Marekani ilitoa wito kwa raia wote wa Tanzania kudumisha umoja,
hekima na amani vilivyoachwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Nyerere.
TEC YALAAMI
Askofu wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC), ambaye pia
ni Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcius Ngalalekumtwa,
alisema kuwa Baraza hilo linalaani tukio hilo la kinyama kwa nguvu zote.
Askofu Ngalalekumtwa alisema kuwa kiongozi wa dini anapotoa kauli ya kulaani basi kauli hiyo inatoka moja kwa moja kwa Mungu.
MUFTI: TUTAJADILI
Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Bin Simba, alisema kuwa tukio
hilo haliwezi kutolewa tamko , kwani inabidi akutane kwanza na Masheikh
ili walizungumzie kwa kina ili wapate kulitolea tamko kali.
Alisema kwamba alikuwa anafanya utaratibu wa kukutana na Masheikh
hao ili wazungumze na kuongeza kuwa hakuna kiongozi yoyote wa dini
atakayelifurahia, na kwamba kiongozi yeyote atakayelifurahia tukio kama
hilo basi huyo siyo kiongozi.
LHRC: POLISI WADHIBITI SILAHA
Polisi wametakiwa kudhibiti uzagaaji wa silaha ili kuepusha matumizi yasiyo sahihi kwa kuteketeza maisha ya raia wasio na hatia.
Mtafiti wa masuala ya haki za binadamu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Pasience Mlowe, alisema:
“Tumesikitishwa sana na tukio hili kwani ni la pili kwa kipindi
kifupi kwenye mkoa huo huo, kama watetezi wa haki za binadamu,
tunalitaka Jeshi la Polisi kudhibiti uzagaaji wa silaha, hizi si bidhaa
zinazoweza kuuzwa ovyo na kila mtu kuwa nazo,” alisema.
Alisema iwapo silaha zitaachwa ziingie kwenye mikoni ya raia
kirahisi, kuna hatari ya watu kuuawa na kujeruhiwa kila mara na
kuonekana ni jambo la kawaida.
Aidha, Mlowe aliwataka wanasiasa kuepuka siasa za chuki
zinazotengeneza sumu miongoni mwa wananchi na badala yake wajinadi kwa
sera za vyama vyao na rasilimali za nchi.
TCD KUKUTANA KUJADILI
Kitio cha Demokrasia Tanzania (TCD), kitakutana mwezi ujao kutafakari kwa pamoja amani ya Taifa ikiwemo tukio la mlipuko huo.
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, alisema jana mjini Dodoma kuwa
katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa amani
ikiwemo mauaji ya watu wenye ulemavu, kwa sababu za kishirikina na
mauaji ya watu mbalimbali.
Aliyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na viongozi wa dini, uchomaji
wa makanisa, kukashifu na kukejeli dini watu wengine, machafuko ya
kutoridhika na matokeo ya chaguzi na migogoro ya ardhi na raia kuuawa
askari wa jeshi la polisi na polisi kuuawa na raia.
Mbatia alisema licha ya matukio hayo kuwa na athari katika usalama
wa taifa, pia yanaweza kusababisha kupunguza mapato nchini yanayotokana
na watalii na kuhoji kuhusiana na majibu mepesi ya serikali kuhusiana na
matukio hayo.
NAPE ADAI CHADEMA INAHUSIKA
Chama Cha Mapinduzi, (CCM) kimelaani tukio hilo na kudai kuwa
Chadema ndiyo wanahusika kutokana na dalili na mazingira yaliyokuwepo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Nape Nnauye, alisema CCM inalaani
tukio hilo na matukio mengine yanayofanana na hayo yaliyotokea nchini.
Alisema kuwa Chadema kinataka umaarufu kupitia matukio na majanga
na kwamba wao ndio wanahusika na urushaji wa bomu hilo kwani kabla ya
kufanyika uchaguzi wa kata, walishasema kama hali ikiwa mbaya kwa
gharama yeyote watahahakikisha uchaguzi wa madiwani katika Mkoa wa
Arusha unaahirishwa.
Hata hivyo, hakuonyesha ushahidi wowote wala kuahidi kuwasilisha ushahidi huo ili kulisaidia Jeshi la Polisi.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment