Thursday, 20 June 2013

KASHFA YA NGONO NAKUMAT SUPERMARKET YACHUKUA SURA MPYA (K’NJARO )


*Meneja wake ataka uchunguzi zaidi ufanyike, na achukuliwe hatua za kinidhamu ikithibitika.

*Awatuhumu wafanyakazi wa kitanzania kwa kuongea sana badala ya kufanya kazi pindi wanaporekebishwa.

*Minong’ono bado yaendelea.

*Hakuna taarifa kwa vyombo husika kushughulikia sakata hilo.
 http://www.arushatimes.co.tz/2011/46/images/695/695%20nakumatt%20moshi.jpg
 
KUFUATIA kashfa ya ngono mahali pa kazi kuikumba Kampuni ya NAKUMAT Moshi, Meneja wa Supermarket hiyo Alfrik Mirimo ametaka uchunguzi zaidi ufanyike.

Itakumbukwa kwamba mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu vyombo vya habari viliripoti kuhusu rushwa ya ngono katika NAKUMAT Supermarket kwa wafanyakazi wa Jinsia ya kike.

Katika ripoti hizo zilisema Meneja wa Kampuni hiyo na baadhi ya wasaidizi wake kutaka kupewa rushwa ya ngono kwa jinsia ya kike pindi watakapo kupandishwa kazi hata kufikia mahali kwa baadhi yao kuacha kazi kwa kutokubali kutoa.

Akizungumza na mtandao huu, Mirimo amesema ripoti hizo zimechafua kampuni yake ya biashara maarufu mjini Moshi ikiwa ni tawi la NAKUMAT Kenya.

Mirimo ametaka uchunguzi zaidi ufanyike kwani katika maeneo ya kazi kuna mambo mengi.
Meneja huyo amesema amekuwa akisuluhisha kesi mbalimbali ndani ya kampuni lake miongoni mwa wafanyakazi wake kuhusiana na vitendo vya ngono.

“Mimi kama baba wa familia, nimekuwa mstari wa mbele kuwalea iweje leo nifanye mwenyewe, nakubali kwamba miongoni mwa wafanyakazi wangu nimekuwa na kazi nzito ya kusuluhisha vitendo vya ngono, kutokana na kuwakiana tama wao kwa wao.” Amesema Mirimo.

“Siwezi kuzuia wao kwa wao kutaka kuingia katika uhusiano wa kimapenzi, sasa nimekuwa nikisuluhisha kutokana na kuonekana kwa visa miongoni mwao labda kukataliwa, lakini mimi sina mazoea na wafanyakazi hata kuniona nimesimama nao, nikitania nao, ukiniona ujue naelekeza tu namna ya ufanyaji kazi.” ameongeza Mirimo. 

mtandao huu,   ukataka kujua endapo itabainika kuwa Meneja huyo amehusika kikamilifu katika vitendo hivyo, Meneja huyo amesema uongozi wa juu wa kampuni hilo umchukulie hatua kutokana na kukiuka makubaliano ikiwezekana kumrudisha nchini Kenya kwa hatua zaidi.

Aidha  mtandao huu, ukataka kujua kutoka kwa Meneja huyo ni utaratibu gani wanautumia kupata wafanyakazi wake na kusema hutangaza nafasi kwa wale waliomaliza kidato cha nne na kuendelea na kuwapatia mafunzo ya ndani kuhusu namna ya kuwahudumia wateja na pindi mfanyakazi anapoonekana kufanya vizuri hupandishwa daraja.

“Inapofikia hatua ya kupandishwa daraja hapo ndipo shughuli huwa pevu hujitokeza ambapo kama nilivyokwambia nimekuwa nisuluhisha kesi hizo kutokana na kuwakiana tamaa; na wanapokataa wanaanza kuchafuana na kujikuta akihusishwa.” Amesema Meneja huyo.

“Nimekuwa Meneja wa Miaka 15 na hii ni kashfa yangu ya kwanza, lakini ninachokiona ni kuwa kitendo cha kuwaajiri watanzania wanawake kumeongeza changamoto kutokana na ukweli kwamba wanaongea sana badala ya kufanya kazi.” Ameongeza Mirimo. 

Hata hivyo  mtandao huu,   umebainika minong’ono kuendelea kuhusu rushwa hiyo ya ngono huku baadhi ya wafanyakazi wa jinsia ya kike wakiwatupia lawama wanawake wenzao kwa kujihusisha na kashfa hiyo ili wapandishwe vyeo.

Minong’ono hiyo imeendelea kudai kuwa kutokana na kiwango kidogo cha elimu na huku maisha yakiendelea kuwa magumu mtaani mtu hujiona ni vyema akajitumbukiza katika rushwa hiyo ili apandishwe daraja kutoka la chini kwenda la juu huku mshahara wake ukiongezeka ili kuweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Aidha hakuna taarifa ya kwamba kashfa hiyo imeripotiwa katika vyombo husika ikiwemo Jeshi la Polisi, TAKUKURU ama Asasi zinazoshughulika na Utetezi wa Haki za Wafanyakazi mahali pa kazi.

Mwandishi: JOHNSON JABIR, Moshi-Kilimanjaro

0 comments: