Friday, 21 June 2013

TAARIFA KUHUSU NASARI, LEMA ,MBOWE NA MAJERUHI WA BOMU

Picture
Jeneza lenye mwili wa Mwenyekiti wa BAWACHA kata ya Sokoni, Judith William Moshi, aliyefariki kwa mlipuko wa bomu kwenye viwanja vya Soweto jijini Arusha siku ya kufunga kampeni za chaguzi ndogo tarehe 15.06.2013.
 
Mtoto Fahad Jamal (7) ambaye hali yake ilikuwa mbaya na kulazwa chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) Hospitali ya Selian, amefariki dunia juzi saa saba mchana hositalini hapo.

Kwa mujibu wa  Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga alisema mtoto huyo alifariki dunia juzi mchana hospitalini hapo wakati  timu ya madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) pamoja na Madaktari wa Jeshi kutoka Hospitali ya Jeshi ya Lugalo wakijaribu kwa kila hali kuokoa uhai wake.

Alisema majeruhi 14 wamelazwa hospitalini hapo huku wengine watatu wakitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Picture
Waombolezaji
Inatipotiwa kwamba askari polisi walivamia nyumbani kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema usiku wa jana kwa lengo la kupekua nyumba yake na kumkamata Mbunge huyo aliyekuwa anatafutwa na polisi.

Taarifa zinasema kuwa Mbunge huyo pamoja na Mbunge mwingine aliyekuwa akitafutwa na jeshi hilo, Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa) tayari wamejisalimisha kwenye ofisi za jeshi hilo asubuhi ya leo kwa ajili ya mahojiano.
Picture
 
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akiwa amelazwa kwenye ndege akifungwa mkanda tayari kwa kusafirishwa kutoka Arusha na kuamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam jana. (picha: Filbert Rweyemamu/MWANANCHI)
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo kutokana na kupigwa na kuumizwa mgongoni na shingoni amehamishiwa kwenye hospitali ya Lugalo ya jijini Dar es Salaam.

“Bunge limegharamia kunisafirisha hadi Muhimbili kwa matibabu zaidi, ofisi ya Bunge ndiyo imetafuta ndege ndogo ya kunipeleka,” alisema Nassari.

Alisema hadi jana alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya mgongo na nyuma ya shingo, ambako alipigwa rungu na vijana wa Kimasai (Morani) na wafuasi wanaodaiwa kuwa wa CCM.

“Baada ya kunipiga nilifanikiwa kutoroka hadi eneo la Minjingu kunusuru maisha yangu, baadaye ilibidi nitafutiwe pikipiki hadi eneo la barabara kuu ndipo niliwakuta askari wa usalama barabarani, waliniombea usafiri hadi hospitali,” alisema Nassari.


0 comments: