Mtoto
mchanga ameliwa na mbwa na kubakishwa mguu, baada ya mtu asiyejulikana
kukitelekeza kichakani katika eneo la Magole, mtaa wa Kivule, Manispaa
ya Ilala, jijini Dar es Salaam.Tukio hilo la kusikitisha limebainika
baada ya mbwa huyo kukibeba kiungo hicho kutoka kilipokuwa na
kukifikisha nyumbani anakofugwa majira ya sita mchana juzi.
Mwenye mbwa huyo aliyejitambulisha kwa jina la Maria John,
aliiambia NIPASHE kuwa, kabla ya kupelekwa mguu huo, jana yake mbwa huyo
alikwenda na utumbo ambao hata hivyo hakuna aliyekuwa na hofu nao,
kwani walidhani ni wa kuku.
“Niliona ni kitu cha kawaida tu, mbwa hutembelea maeneo mbalimbali
labda ameokota mzoga wa kuku, lakini leo (juzi) nilipoona mguu
nilistaajabu na kufahamu kuwa ni kiungo cha binadamu nilitoa taarifa kwa
majirani na kupata msaada,” alisema.
Alisema lengo la kutoa taarifa kwa majirani zake ni ili waweze
kujadiliana na kutamfuta aliyefanya kitendo hicho cha kikatili kisha
baadaye kutoa taarifa kwa mjumbe wa mtaa huo.
Mmoja wa majirani waliokusanyika kushuhudia tukio hilo ambaye
hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema hajawahi kushuhudia
tukio kama hilo.
“Ni tukio la kushangaza na kusikitisha sana kwa mtu kukatisha
maisha ya kiumbe kisicho na hatia,kwani huwezi kujua mungu alimpangia
nini duniani, hivyo kwa kweli kama mama najisikia uchungu sana,”
alisema.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa eneo hilo, Grace Martin, alisema
alipigiwa simu na mdogo wake kuwa, mbwa ameokota kiungo cha mtoto na
kutakiwa kurudi mtaani hapo haraka.
“Nilipofika nilihakikisha kuwa kweli ni mguu wa mtoto, niliamua kumpigia simu Mwenyekiti wa Mtaa kwa ajili ya msaada,”alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule,Joseph Gassaya alisema
yeye alipojulishwa alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kituo cha
Stakishari Ukonga nao baada ya muda mfupi walifika eneo la tukio.
Alisema askari walitoa amri ya kukizika kiungo hicho katika eneo
hilo, huku Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wa kumsaka mama
aliyefanya ukatili huo ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
SOURCE:By Leonce Zimbandu
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment