Sunday, 16 June 2013

MIAKA 67 JELA KWA NJAMA ZA KUPORA PESA NMB BANK

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Moshi, mkoani Kilimanjaro imewahukumu raia wawili wa Kenya na mwanamke mmoja Mtanzania jela miaka 67 baada ya kupatikana na hatia ya kula njama na kupora Sh milioni 239 kutoka benki ya NMB tawi la Mwanga, Kilimanjaro.

Uporaji huo ulifanyika Julai 11, 2007 ambapo pia watu hao waliiba bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) mali ya Jeshi la Polisi nchini, na kumuua askari Polisi Michael Milanzi aliyekuwa lindo.

Watuhumiwa hao waliofungwa ni Samweli Gitau maarufu kwa jina la Saitoti na Michael Joseph Kimani (wote kutoka Kenya) na Mtanzania Elizabeth Elias maarufu kwa jina la Bella mkazi wa Kwangulelo mkoani Arusha.

Jopo la makakimu watatu wakiongozwa na Panterine Kente liliwahukumu kwenda jela miaka saba kwa 
kosa la kwanza ambalo ni kula njama; miaka 30 kila mmoja kwa kosa la uporaji pamoja na miaka 30 kwa kosa la wizi wa silaha.

Hakimu huyo alisema kuwa adhabu hizo zinaenda pamoja hivyo washitakiwa watatumikia kifungo cha miaka 67 jela, mbali na hukumu hiyo Mahakama hiyo pia iliwaachia huru ndugu watatu ni ambao ni Devotha Elias Masenza, Ntibasana Elias Masenza na Julian Elias Masenza na mtu mwingine Calist Kanje baada ya ushahidi dhidi yao kushindwa kuishawishi Mahakama.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo , wakili wa Serikali Tamali Mndeme aliomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.

---
Imeandikwa na Tamimu Adam
Jeshi la Polisi, Moshi
Chanzo HabariLeo

0 comments: