Thursday, 20 June 2013

RAIS MSTAAFU GEOGE W.BUSH KUHUTUBIA WAKE WA MARAIS WA AFRIKA DAR

RAIS mstaafu wa Marekani, George W. Bush na mkewe, Laura, wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi ujao ambapo watahutubia kongamano litakalojadili wajibu wa wake za marais katika kuinua wanawake duniani.

Taasisi ya George Bush ndiyo imeandaa kongamano hilo litakalofanyika Dar es Salaam kuanzia Julai 2 hadi 3.

Taarifa iliyotolewa jana na taasisi hiyo kwa vyombo vya habari, ilisema kongamano hilo, litahudhuriwa pia na mke wa Rais Barack Obama wa Marekani, Michelle na muasisi wa Taasisi ya Wanawake ya Cherie, Cherie Blair ambaye ni mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair.

Wake wengine wa marais wa Afrika watakaohudhuria ni Mama Salma Kikwete, Chantal Campaore wa Burkina Faso, Roman Tesfaye wa Ethiopia, Maria da Luz Dai Guebuza (Msumbiji), Penehupifo Pohamba (Namibia), Sia Nyama Koroma (Sierra Leone), Janet Museveni (Uganda) na Christine Kaseba wa Zambia.

Kongamano hilo litajikita zaidi katika kujadili masuala ya kuwekeza kwa wake, kuimarisha Afrika lakini pia wajibu wa wake za marais kuhamasisha wanawake katika maeneo ya elimu, afya na kuwakwamua kiuchumi.

“Kongamano hili litakutanisha pamoja wake za marais, maofisa wa Serikali, mashirika binafsi, Asasi Zisizo za Serikali (AZISE) na wasomi kujadili mambo muhimu ya kuchukuliwa hatua ili kunufaisha wanawake,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika kongamano hilo ni kuinua wajasiriamali wanawake kiuchumi kupitia mafunzo na teknolojia, kupatia fursa wanawake wakulima kwa kupewa mafunzo ya kilimo cha kisasa, mafunzo kuhusu saratani ya matiti na umuhimu wa elimu kwa wanawake.

Kongamano hilo linafanyika sambamba na ujio wa Rais Obama anayetarajiwa kuwasili nchini mwanzoni mwa mwezi ujao.


 

0 comments: