Tuesday, 11 June 2013

KADINALI PENGO NA IGP MWEMA WAPIGA VITA UHALIFU NCHINI


1Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema akiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Kardinali Pengo wakiingia katika ukumbi wa mkutano wakati wa kikao cha Mashauriano kati ya Jeshi la Polisi na viongozi wa makanisa ya kikatoliki uliofanyika jijini Dar es Salaam.(Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)4
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini , IGP Said Mwema akizungumza katika kikao cha Mashauriano kati ya Jeshi la Polisi na viongozi wa makanisa ya kikatoliki.kikao hicho pia kilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Kardinali Pengo .Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam.(Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
 
Imeelezwa kuwa Viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika jamii ya kupunguza uhalifu kwa kuwa wao wanauwezo wa kuwabadili watu kimatendo na kifikra  kwa kufanya doria ya mwili na roho kwa pamoja hivyo wanaweza kusaidiana na Polisi katika kupunguza uhalifu.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa mashauriano baina ya Jeshi la Polisi na Viongozi wa dhehebu la Romani Katoliki uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinali Pengo.
Mwema alisema katika kipindi hiki viongozi wa dini pamoja na Jeshi la Polisi wanatakiwa kula njama ya kupambana na uhalifu kwa kuhakikisha kuwa wahalifu wote wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria na Viongozi wa dini wanatakiwa watumie nafasi walizonazo katika kuhakikisha kuwa waumini wao wanajua mbinu za kujilinda na kuhakikisha taifa linakuwa salama.
Aidha amewataka kutumia takwimu za uhalifiu zinazotolewa na Jeshi la Polisi katika kazi zao za kila siku ili kuhakikisha kuwa wale wahalifu wote wanaacha kutenda vitendo hivyo na wanarejea katika nyumba za ibada na kuwa watu wema.
 Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam Mwadhama Kardinal Pengo amesema viongozi wa dini hawawezi kukwepa jukumu lao la kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua hapa nchini kwa kuwa jukumu hilo linaanzia kwao.
Pengo alisema kuongezeka kwa uhalifu ni changamoto kwa viongozi wa dini kwa kuwa wao ndio wenye kazi ya kujenga maadili katika jamii na polisi kusimamia sheria na kuwachukulia hatua wale wanaokaidi
Akisoma maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Mhashimu Eusebius Nzigilwa alisema wamekubaliana kuziimarisha kamati za ulinzi na usalama katika nyumba za ibada zilizopo hivi sasa wakati wakiendelea kupata mafunzo ya ukamataji salama kutoka Jeshi la Polisi.
“Parokia ambazo hazijaunda kamati za ulinzi na usalama zihakikishe zinafanya hivyo ndani ya mwezi huu na zile ambazo zimeundwa lakini hazifanyi kazi mziimarishe ili kwa pamoja tuwe salama katika nyumba zetu za ibada”Alisema Askofu Nzigilwa.
 
Chanzo  francisgodwin blog

0 comments: