Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania
kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya
Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali
ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
Tenga,
ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, alisema
tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa
zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika
wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali
inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko.
“Masuala
ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa
hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri,
itaruhusu,” alisema Tenga.
“Jukumu
la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na
Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.
“Kama
tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja
zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha
ya wananchi wake.”
Tenga
alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika
za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo
Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.
Alisema
wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu
(FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na
kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha
Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa
usalama.
Hivyo
nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama,
lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur,
hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana
kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.
Alisema
watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.
“Mhe.
Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni
nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati
hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.
“Kwa
maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali
itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni
kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza
tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”
Alifafanua
kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama
cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.
“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya
Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo
yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,”
alisema.
“Sasa
ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende
kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
0 comments:
Post a Comment