YANGA SC imevunja kambi yake na wachezaji wamepewa
mapumziko ya wiki mbili, baada ya Serikali kuzuia timu za Tanzania kwenda Sudan
kushiriki Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Mabingwa
hao watetezi wa Kagame mara mbili mfululizo na mara tano jumla, (1975, 1993,
1999, 2011 na 2012) hawatashiriki tena mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza
la Vyama Soka Afrika Mashariki Kati (CECAFA) yaliyopangwa kuanza kutimua
vumbi nchini Sudan Jumanne wiki ijayo, Juni 18.
Yanga
haitashiriki mashindano hayo kufuatia kauli ya Serikali juu ya kutozirushu timu
zake kwenda kwenye mashindano hayo kutokana na hofu ya usalama kwa wachezaji na
viongozi wakati wa mashindano hayo.
Mapema
jana Bungeni, Dodoma, Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makalla
alisema hali ya usalama katika miji ya El- Fashir na Kadugli sio nzuri,
Serikali haitaziruhusu timu za Tanzania kwenda kushiriki michuano hiyo.
“Sehemu
ambayo mashindano yanafanyika hakuna usalama wa kutosha, mwisho kutembea saa 12
jioni, huduma za hoteli ni duni hazijitoshelezi kuweza kukaa kwa timu katika
miji hiyo na kubwa zaidi ni hali ya usalama, kutoka Khartoum mpaka Al Fashir
inabidi kutumia usafiri wa Helikopta kitu ambacho bado ni hatari,” alisema
Makalla.
Kocha
Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts amepongaza Serikali kwamba imetazama
mbali na kuona umuhimu wa usalama kwa watu wake, kwani hawawezi kucheza
michuano zaidi ya wiki mbili katika maeneo yanayolindwa na vikosi vya majeshi
ya ulinzi na usalama kutoka nchi mbalimbali.
Yanga
ilianza mazoezi wiki iliyopita Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es
Salaam kujiandaa na mashindano hayo, sasa itajikusanya tena baada ya wiki mbili
kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
0 comments:
Post a Comment