MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imewahukumu kifungo cha miaka
mitano jela askari saba wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma ambao walikuwa
wakishtakiwa kwa mauaji.
Akitoa hukumu yake katika
kikao cha Mahakama Kuu kilichokuwa kikifanyika mkoani Kigoma Jaji wa
mahakama hiyo, Sam Mpaya Rumanyika alisema kuwa baada ya kupitia
ushahidi mbalimbali Mahakama hiyo imewatia hatiani askari hao kwa kosa
la kuua bila kukusudia.
Katika kesi hiyo namba
35 ya mwaka 2012 washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na
kusomewa shitaka la kumuua Festo Stephano, mkulima wa kijiji cha Rungwe
Mpya Wilaya ya Kasulu mkoani hapa katika tukio lililotokea Agosti 6,
mwaka 2011.
Askari hao waliohukumiwa ni pamoja
na Baraka Hongdi, Koplo Mawazo, Koplo Swahib, D/C Charles, D/C Shamsi,
D/C Jerry na D/C Amrani ambao kwa pamoja walikana shitaka lao katika
kesi hiyo namba 35 ya mwaka 2012.
Akitoa
utetezi kabla ya hukumu hiyo wakili wa washitakiwa, Method Kabuguzi
aliiomba Mahakama kuwafutia shitaka washitakiwa hao na kuwaachia huru
kwani wote bado vijana na wameoa hivi karibuni.
Sambamba
na hilo Kabuguzi alisema kuwa askari hao walikumbwa na mkasa huo wakati
wakitekeleza jukumu lao la ulinzi wa taifa ambapo walimkamata mtuhumiwa
wa kutumia silaha na ndipo kifo kikatokea wakati wakitekeleza majukumu
yao.
0 comments:
Post a Comment