TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
09/06/2013
MAONI YA AWALI YA MWENYEKITI WA CUF KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA
09/06/2013
MAONI YA AWALI YA MWENYEKITI WA CUF KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA
UTANGULIZI;
Kwanza naipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kazi kubwa waliofanya ya kuratibu maoni na kuja na mapendekezo ya katiba mpya ambayo hayakushinikizwa na matakwa ya Chama tawala cha CCM. Tume imeonyesha ujasiri mkubwa na hakika wahafidhina wa chama hicho watachukia sana.
Mambo mengi yaliyopendekezwa na Chama Cha Wananchi CUF yameingizwa katika Rasimu ya Katiba. Mambo hayo ni pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu, kuruhusiwa mgombea binafsi, Rais kutangazwa kushinda akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wale wawili walio ongoza kwa kura, Tume huru ya uchaguzi, Mawaziri kutokuwa wabunge, Spika kutokuwa mbunge, haki za watu wenye ulemavu, haki za binadamu na mengine mengi.
Hata hivyo mambo mengi muhimu kama vile umilikaji wa ardhi, maliasili na rasilimali za nchi kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote, elimu, afya, mazingira ya kukuza uchumi unaoleta neema kwa wananchi wote, wajibu, uwezo na uhuru wa serikali za mitaa hayajaingizwa ndani ya katiba kikamilifu kwani rasimu ya katiba imeshughulikia mambo ya muungano.
Mambo ya Muungano ni saba: Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa
Vyama vya Siasa na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mwongozo wa Tume kuhusu utoaji wa maoni ulijikita katika maeneo yafuatayo; Misingi na Maadili ya Kitaifa, Madaraka ya Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Haki za Binadamu na Wajibu wa Wananchi, Ardhi, Maliasili na Mazingira, Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu na Utawala), Mihimili ya Utawala (Serikali, Bunge na Mahakama), Serikali za Mitaa, Muundo na Mamlaka yake, Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Mambo mengi muhimu kwa mwananchi wa kawaida ikiwa ni pamoja na serikali za mitaa, umilikaji wa ardhi, haki za huduma za afya na elimu, na matumizi ya maliasili hayajaingizwa katika katiba hii na yanatarajiwa kuingizwa kwenye katiba ya Tanzania Bara. Rasimu ya katiba kwa wananchi wa Tanzania Bara haijakamilika mpaka Rasimu ya katiba ya Tanzania Bara itakapokuwa tayari. Hotuba ya uzinduzi wa katiba ya Jaji Warioba haikulifafanua suala hili. Hakuna mantiki ya kupigia kura ya maoni katiba ya jamhuri ya muungano bila kuwa na katiba ya Tanzania Bara kwa upande wa bara na marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na katiba ya jamhuri ya muungano kwa upande wa zanzibar. Katiba ya Tanzania Bara na katiba ya Zanzibar iwe ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kuwepo kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara kutasaidi kuondoa kuweka asasi mbili au tatu zinazofanya kazi moja. Kwa mfano Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ya serikali ya Muungano ikafanya kazi pia kwa serikali ya Tanzania Bara ikiwa wananchi wa Tanzania Bara hawana tatizo na utaratibu huo.
MAPENDEKEZO YA JUMLA;
Haya ni mapendekezo ya awali tu, mapendekezo mengine yataendelea kutolewa kwa kadri ambavyo tutazidi kuichambua rasimu hii ya katiba. Natoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha kuwa wanaitafuta rasimu hii bila kuchoka, kuisoma na kuielewa na kuendelea kutoa mapendekezo yao kwa tume ya mabadiliko ya katiba iwe ndiyo lengo kuu.
Kwa sababu tume imetangaza kuwa itachapisha rasimu katika magazeti ya serikali kwa maana ya HABARI LEO na ZANZIBAR LEO, tunaona kama huku ni kuififisha rasimu isiwafikie watanzania wengi zaidi.
Kuna haja ya dhati, tume ikaitangaza rasimu katika magazeti mbalimbali ya kila wiki na ya kila siku ili kuhakikisha kuwa rasimu imefikiwa na imesomwa na watanzania wengi. Na nakala zitakazobakia “returns” baada ya mauzo ya magazeti husika tume izinunue nakala hizo na izisambaze kwa utaratibu maalum mikoani na vijijini.
Ni ushauri wetu kwa Tume pia kwamba baada ya kazi kubwa waliyoifanya, wasikubali kuyumbishwa na wahafidhina wasiopenda mabadiliko wanaotokana na CCM. Tume iwe na msimamo na iangalie wananchi wanataka nini na itetee masuala ya msingi na ya maslahi ya wananchi ambayo inaona ni muhimu yakatetewa kwa maslahi ya taifa na hasa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi.
Na mwisho, Tume ihakikishe kuwa masuala haya tunayoyashauri kwa awamu yanapewa uzito na tafakuri pana ili kuipata katiba itakayokuza uchumi imara, kuongeza ajira kwa vijana na kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
“Mungu Ibariki Tanzania”
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.
Mwenyekiti,
09 Juni 2013, Dar Es Salaam.
Mwongozo wa Tume kuhusu utoaji wa maoni ulijikita katika maeneo yafuatayo; Misingi na Maadili ya Kitaifa, Madaraka ya Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Haki za Binadamu na Wajibu wa Wananchi, Ardhi, Maliasili na Mazingira, Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu na Utawala), Mihimili ya Utawala (Serikali, Bunge na Mahakama), Serikali za Mitaa, Muundo na Mamlaka yake, Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Mambo mengi muhimu kwa mwananchi wa kawaida ikiwa ni pamoja na serikali za mitaa, umilikaji wa ardhi, haki za huduma za afya na elimu, na matumizi ya maliasili hayajaingizwa katika katiba hii na yanatarajiwa kuingizwa kwenye katiba ya Tanzania Bara. Rasimu ya katiba kwa wananchi wa Tanzania Bara haijakamilika mpaka Rasimu ya katiba ya Tanzania Bara itakapokuwa tayari. Hotuba ya uzinduzi wa katiba ya Jaji Warioba haikulifafanua suala hili. Hakuna mantiki ya kupigia kura ya maoni katiba ya jamhuri ya muungano bila kuwa na katiba ya Tanzania Bara kwa upande wa bara na marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na katiba ya jamhuri ya muungano kwa upande wa zanzibar. Katiba ya Tanzania Bara na katiba ya Zanzibar iwe ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kuwepo kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara kutasaidi kuondoa kuweka asasi mbili au tatu zinazofanya kazi moja. Kwa mfano Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ya serikali ya Muungano ikafanya kazi pia kwa serikali ya Tanzania Bara ikiwa wananchi wa Tanzania Bara hawana tatizo na utaratibu huo.
MAPENDEKEZO YA JUMLA;
- Pendekezo langu la msingi ni kwamba, kura ya maoni isubiri kukamilishwa kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara na zote zikajadiliwa na wananchi kwa pamoja. Sina pingamizi kuwa Wajumbe wa Tume wa Tanzania Bara waandae rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara, na wajumbe wa Zanzibar waandae mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya Zanzibari ili isikinzane na katiba ya Jamhuri ya Muungano. Muda wa kuyatekeleza haya na kubadilisha sheria zifuate matakwa ya katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 haupo. Serikali imeeleza kuwa haina nia na Rais Kikwete hataki kabisa kujiongezea muda kwa kisingizio cha kukamilisha utaratibu wa katiba mpya. Wananchi pia wamechoka wanataka mabadiliko.
- Katika masuala ya haki za binadamu ningependa Katiba itamke wazi kuwa mwanamke mjamzito ana haki ya kupata lishe bora na huduma za afya wakati wa ujauzito na kujifungua. Vile vile watoto bila kujali uwezo wa wazazi wao wana haki ya lishe bora, huduma za msingi za afya na elimu inayomuandaa mtoto kukabiliana na changamoto za maisha.
- Pendekezo la Rasimu ya Katiba ya kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi ni la msingi. Pendekezo hili lianze kufanyiwa kazi mara moja ili kufanya mabadiliko ya sheria ya uchaguzi na Tume ya uchaguzi ili uchaguzi wa 2015 uendeshwe na Tume iliyo Huru kweli. Mchakato wa mabadiliko ya katiba utaendelea baada ya uchaguzi mpaka ukamilike na sheria husika kufanyiwa mabadiliko.
- Siyo lazima Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wawe watu waliyewahi kushika wadhifa wa Jaji wa Makakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu na ameshika wadhifa huo kwa kipindi kisichopungua miaka mitano kama Rasimu ya Katiba inavyoelekeza katika kifungu 181(4). Masuala ya kusimamia uchaguzi ni ya utawala na uendeshaji kuliko ya kutafsiri sheria. Majaji siyo wasimamizi na mameneja wazuri wa utawala na logistics. Nchini Ghana mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ambaye kafanya vizuri siyo Jaji bali ni Profesa wa sayansi ya siasa – Jaji Lewis Makame kwa miaka zaidi ya 15 na hakufanikiwa kujenga Tume ya Uchaguzi yenye uwezo na kuaminika. Ni vyema wigo wanaoweza kuomba kuwa wenyeviti wa Tume ukapanuliwa na kuingiza wenye uzoefu wa utawala na logistics. Tume ina mwanasheria wake ambaye ataelekeza na kushauri masuala yahusiyo sheria.
- Kasoro kubwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni kwamba haina nyenzo za kutimiza malengo muhimu ya katiba yenyewe. Ibara ya 6(b) imeeleza kuwa “lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi.” Mambo ya uchumi yote isipokuwa Benki Kuu na sarafu hayamo katika orodha ya mambo ya Muungano. Hata suala la uratibu wa sera za uchumi halimo. Ibara ya 7(2) inaeleza “mamlaka ya nchi na vyombo vyake vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote kwa lengo la kuhakikisha kwamba: (c)Serikali itahakikisha kuwa shughuli zinazofanywa zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (d)ardhi ikiwa rasilimali kuu na msingi wa Taifa, inalindwa, inatunzwa na kutumiwa na wananchi wa Tanzania kwa manufaa, maslahi na ustawi wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo; (e)maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na kukuzwa kwa ulinganifu na kwa pamoja na kwa namna ambayo inawanufaisha wananchi wote; (f)kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu kipato chake; (j)utajiri wa rasilimali na maliasili za Taifa unaelekezwa katika kuleta maendeleo, kuondoa umaskini, ujinga na maradhi”. Serikali ya Muungano haina nyenzo ya kusimamia mambo hayo.
- Ibara ya 11 inazungumzia utekelezaji wa malengo ya taifa. Kifungu (2) kinaeleza “Serikali itatoa taarifa Bungeni si chini ya mara moja katika kila mwaka, kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka ya nchi ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa yaliyoainishwa katika Katiba hii. (c) kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili: (i) kuwaletea wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini; (ii) kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (iii) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi; (iv) kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kukuza fursa za uwekezaji; (v) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao; (vi) kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na uendelezaji wa masoko ya mazao yao; (vii) kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji wa mizania ya bei za mazao na pembejeo; (viii) kuimarisha na kuendeleza uwekezaji wa ndani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, maeneo ya ufugaji na vifaa vya uvuvi; (ix) kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fursa na nafasi za wazi kwa watu wote na kuanzisha shughuli za kiuchumi na kukuza mazingira yaliyo bora kwa ajili ya kuhamasisha sekta binafsi katika uchumi; (x) kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa maana ya kufanya shughuli yoyote halali inayompatia kipato; (xi) kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa huru kupata fursa sawa ya kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake. Mambo yote haya siyo ya muungano”. Serikali ya Muungano itawezaje kutoa taarifa Bungeni kwa mambo ambayo haiyasimamii.
- Ukizingatia mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa na Rasimu, Serikali ya Muungano haina vyanzo vya mapato ya kodi. Ibara ya 215 imeeleza Vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakuwa:“(a) ushuru wa bidhaa; (b) maduhuli yatokanayo na taasisi za Muungano; (c) mchango kutoka kwa Washirika wa Muungano; na (d) mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano”. Katiba haizungumzii taasisi yeyote ya kukusanya kodi. Jambo la saba la muungano ni Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano. Mambo sita ya Muungano hayalipi ushuru wa bidhaa. Biashara siyo jambo la Muungano kwa hiyo ushuru wa forodha, kodi za ongezeko la thamani (VAT), excise duty, kodi ya mauzo haziwezi kuwa suala la Muungano. Mwaka wa fedha wa 2010/11 Mapato ya serikali Asilimia 34.3 ushuru wa forodha na VAT katika bidhaa zinazoagizwa toka nje, Asilimia 18.6 kodi (VAT na Excise duty) za bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Asilimia 29 kodi ya mapato. Kodi na tozo nyingine asilimia 10.5, Mapato ya halmashauri asilimia 2.8. Kodi ni chanzo cha mapato ya serikali lakini pia ni sera ya uchumi. Viwango gani vya kodi havina athari kubwa kwa wananchi maskini na kupunguza motisha ya uzalishaji na uwekezaji? Serikali za washirika wa Muungano hawatakubali Serikali ya Muungano kutoza kodi katika maeneo ambayo siyo ya muungano. Katiba haina muongozo wowote wa michango toka washirika wa Muungano. Rasimu hii ilivyo ikipitishwa kutakuwa na mgogoro mkubwa wa fedha za kuendeshea serikali ya Muungano na hatma yake itakuwa Muungano kuvunjika.
- Katika mambo ya uchumi Tume haikufanya uchambuzi wa kina wa kuwa na katiba inayojenga mazingira mazuri ya kukuza uchumi unaoleta maendeleo kwa wote. Katiba haiibani serikali iwe na utaratibu mzuri wa bajeti. Katika mambo ya usimamizi wa matumizi ya serikali na kazi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali rasimu hii ime –“copy” na ku-“paste” katiba ya sasa bila kutathmini kama mfumo wa hivi sasa unafanya kazi. Eneo hili linahitaji kufanyiwa uchambuzi zaidi.
- Ibara za 213 na 214 zinawapa uwezo Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mshirika wa Muungano “zitakuwa na mamlaka ya kukopa fedha ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kugharamia shughuli zilizo chini ya mamlaka yake.” Katika utaratibu huu nchi inaweza kughubikwa na madeni ikiwa serikali tatu zitashindana kukopa ndani na nje ya nchi. Lazima pawe na mwongozo wa kudhibiti mikopo na kuongezeka kwa deni la taifa. Nchi inaweza kuingizwa katika mgogoro wa madeni. Uhuru wa serikali zote tatu kukopa ndani na nje ya nchi inaweza kusababisha kukua kwa madeni kupita kiasi. Serikali za washirika zina vyanzo vya mapato serikali ya muungano haina. Kwa Rasimu ya Katiba hii serikali za washirika ndizo zinazokopesheka na siyo serikali ya muungano.
- Rasimu ya Katiba bila kusema hivyo inapendekeza kuwepo na Benki Kuu tatu. Ibara ya 217 inaeleza“Kutakuwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayojulikana kuwa “Benki Kuu” ambayo itakuwa na majukumu yafuatayo: (a) kutoa sarafu, kudhibiti na kusimamia mzunguko wa sarafu; (b) kuandaa na kusimamia Sera na Mipango inayohusiana na sarafu; (c) kudhibiti na kusimamia masuala ya fedha za kigeni; na (d) kusimamia Benki za Washirika wa Muungano.” Ibara ya 218 inaeleza “Serikali za Washirika zitakuwa na Benki zitakazokuwa najukumu la kutunza akaunti ya fedha za Serikali husika, kusimamia Sera za Kifedha na benki za biashara katika mamlaka zao.” Kazi ya Benki Kuu ni kusimamia Benki za Biashara, sera za fedha na hasa riba, na mfumo wa malipo. Kazi hizi zitafanywa na Benki za Washirika wa Muungano.Moja ya chanzo cha mgogoro wa Euro ni kutokuwepo usimamizi wa pamoja wa Benki za biashara. Hivi sasa Ukanda wa Euro unajaribu kuandaa utaratibu wa pamoja wa kuifanya Benki Kuu ya Ulaya (ECB) kusimamia Benki za Biashara. Kama tuna sarafu moja tuwe na Benki Kuu moja. Benki Kuu isiposimamia benki za biashara haitaweza kudhibiti na kusimamia ujazi wa fedha (money supply)
- Ibara ya 105 inaeleza “(2) Wajumbe wa Bunge watakuwa wa aina zifuatazo: (a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi; (3) Kwa madhumuni ya Ibara ya ndogo (2)(a), kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa ni jimbo la uchaguzi”. Nini vigezo vya kufanya mikoa na wilaya kuwa majimbo ya uchaguzi? Utaratibu wa kuanzisha mikoa na wilaya ni wa serikali washirika au wa Serikali ya Muungano? Hata hivyo ibara ya 180 (a) inaeleza “mamlaka zinazosimamia uchaguzi kutangaza majimbo kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge.” Majimbo ya uchaguzi yataundwa na Tume au tayari yameishatajwa na katiba?
- Mamlaka ya Bunge katika kuisimamia serikali katika masuala ya bajeti ni madogo. Ibara ya 107 (2) inaeleza, “katika kutekeleza majukumu yake, Bunge litakuwa na madaraka yafuatayo: (c) kujadili mgawanyo na kuidhinisha matumizi ya fedha kwa Wizara, taasisi na mashirika ya Serikali; (d) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti; (e) kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika Jamhuri ya Muungano; (f) kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi”. Hata hivyo Mambo ya Muungano hayahusishi Mpango wa Maendeleo wa taifa.
- Ibara ya 177 inaeleza “Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii, utumishi wa umma na uongozi katika Jamhuri ya Muungano utazingatia misingi kwamba utoaji wa ajira na uteuzi wa viongozi utakuwa kwa uwiano baina ya Washirika wa Muungano, kwa kuzingatia weledi na taaluma katika eneo au nyanja husika.” Nini maana ya uwiano? Je maana yake nusu ya wafanyakazi watoke Zanzibar na nusu watoke Tanzania Bara?
- Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ni muhimu iwemo ndani ya Katiba. Rasimu haina asasi hii muhimu ya usimamizi na uwajibikaji. Tunarudia pendekezo letu kuwa Katiba ieleze kuwepo kwa Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na kueleza kazi zake. Tume hii iwe na uhuru wa kupeleka kesi mahakamani bila idhini ya Mkurungezi wa Mashtaka ya Umma (DPP).
- Katiba imejaa imani kuwa vyeti vya shule na vyuo ndiyo elimu na hekima na kwa kutumia sifa za vyeti vya elimu inawanyima haki wananchi wengi kushiriki na kuwania uongozi katika ngazi mbalimbali. Ibara ya 75(f) inaeleza sifa moja ya Rais kuwa “anayo angalau shahada ya kwanza ya chuo kikuu kinachotambuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.” Cheti cha shahada siyo kipimo kizuri cha elimu, hekima na uwezo wa kuongoza. Bill Gates hakumaliza masomo yake ya shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Harvard. Aliona anapoteza muda akaanzisha kampuni ya Microsoft. Kama Bill Gates angekuwa Mtanzania, Rasimu ya Katiba ingemzuia kugombea Urais kwa kuwa hana cheti cha shahada. Steve Jobs pia hakumaliza na kupata shahada badala yake alifanya masomo aliyoyaona muhimu na kuanzisha kampuni ya Apple. Hapa Tanzania sidhani kama Said Salim Bakhresa ana shahada yeyote. Taarifa iliyoko Wikipedia na gazeti la Forbes inaeleza aliacha shule akiwa na miaka 14 na akaanza biashara ya kuuza potato mix. Kama taarifa hii ni kweli basi huenda hata darasa la 8 hakumaliza. Lakini uwezo, uzoefu na elimu itokanayo na uzoefu wa kazi ni kubwa kuliko hata mtu mwenye PhD ya biashara. Mzee Bakhresa hana sifa ya kugombea Urais kwa kuwa hana shahada ya kwanza. Sina uhakika kama Freeman Mbowe ana shahada. Ikiwa hana siyo haki kumzuia kugombea Urais kwa sababu hiyo. Mwache agombee na wengine wajenge hoja hana maadili na uwezo wa kuongoza nchi. John Major alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwaka 1991 – 97 hana shahada ya Chuo Kikuu. Kuna watu wengi wenye shahada nyingi lakini hawana hekima wala busara. Vyeti vingi vys siku hizi ni vya kughushi na inawezakana kabisa usiweze kugundua kuwa vimeghushiwa. Sifa ibakie kusoma na kuandika kiswahili. Wache wapiga kura waamue kuwa elimu ya mgombea haitoshi kumfanya kuwa Rais. Sifa ya elimu ya mgombea ubunge ni kidato cha nne. Rasimu itamzuia Mzee Bakhresa hata kugombea ubunge kwa sababu hana cheti cha kidato cha nne. Kuna Watanzania wengi waliomaliza darasa la nane au la saba la zamani wenye elimu bora kuliko aliyemaliza kidato cha nne hivi karibuni. Kuna watu wengi wamemaliza darasa la 7 wana uzoefu mzuri na wana uwezo wa kuwawakilisha wananchi katika Bunge. Vigezo vya vyeti vya elimu visitumiwe kuwanyima wananch haki zao za kisiasa. Kigezo cha shahada pia kimeingizwa katika uteuzi wa Mawaziri. Watu wenye uzoefu na uwezo wa uongozi lakini hawana vyeti vya shahada hawawezi kuteuliwa kuwa mawaziri. Nastaajabu hii obsession na vyeti imetoka wapi?
- Ibara ya 31 inazungumzia Dini. “(1) Kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya imani ya dini na anao uhuru pia wa kubadilisha dini, imani yake au kutokuwa na imani na dini. Kifungu cha (5) Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini nyingine, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini”. Tatizo ya ibara hii ni tafsiri ya kukashifu. Imani za dini zina tofauti. Imani ya msingi ya dhehebu moja inaweza kuwa kufuru kwa dhehebu lingine na ikatafsiriwa kuwa ni kukashifu. Kuna masuala ambayo jamii inapaswa kujenga maelewano ya kuvumiliana na kuheshimiana na kukubali tofauti za imani bila kugombana. Kuliweka katika katiba inaweza kujenga chuki na ikatafsiriwa kuwa inalenga kundi fulani. Ibara na 5 imelenga kikundi au taasisi ya dini. Je vikundi ambavyo siyo vya dini vinaruhusiwa kukashifu imani na dini?
- Serikali ya Muungano itakuwa na Jeshi la ulinzi, Polisi na Usalama wa Taifa. Serikali za washirika zinaruhusiwa kuwa na polisi na usalama wa taifa. Inawezekana serikali ya Muungano ikaongozwa na Chama A, Serikali ya Zanzibar ikaongozwa na chama B na serikali ya Tanzania Bara ikaongozwa na chama C. Serikali zote zina polisi na usalama wa taifa wake, haitakuwa kasheshe ndani ya nchi? Sina uhakika katiba imeweka bayana utaratibu wa kuzuia migongano kati ya vyombo vya Muungano na vyombo vya Washirika.
Haya ni mapendekezo ya awali tu, mapendekezo mengine yataendelea kutolewa kwa kadri ambavyo tutazidi kuichambua rasimu hii ya katiba. Natoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha kuwa wanaitafuta rasimu hii bila kuchoka, kuisoma na kuielewa na kuendelea kutoa mapendekezo yao kwa tume ya mabadiliko ya katiba iwe ndiyo lengo kuu.
Kwa sababu tume imetangaza kuwa itachapisha rasimu katika magazeti ya serikali kwa maana ya HABARI LEO na ZANZIBAR LEO, tunaona kama huku ni kuififisha rasimu isiwafikie watanzania wengi zaidi.
Kuna haja ya dhati, tume ikaitangaza rasimu katika magazeti mbalimbali ya kila wiki na ya kila siku ili kuhakikisha kuwa rasimu imefikiwa na imesomwa na watanzania wengi. Na nakala zitakazobakia “returns” baada ya mauzo ya magazeti husika tume izinunue nakala hizo na izisambaze kwa utaratibu maalum mikoani na vijijini.
Ni ushauri wetu kwa Tume pia kwamba baada ya kazi kubwa waliyoifanya, wasikubali kuyumbishwa na wahafidhina wasiopenda mabadiliko wanaotokana na CCM. Tume iwe na msimamo na iangalie wananchi wanataka nini na itetee masuala ya msingi na ya maslahi ya wananchi ambayo inaona ni muhimu yakatetewa kwa maslahi ya taifa na hasa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi.
Na mwisho, Tume ihakikishe kuwa masuala haya tunayoyashauri kwa awamu yanapewa uzito na tafakuri pana ili kuipata katiba itakayokuza uchumi imara, kuongeza ajira kwa vijana na kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
“Mungu Ibariki Tanzania”
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.
Mwenyekiti,
09 Juni 2013, Dar Es Salaam.
0 comments:
Post a Comment