WACHEZAJI na viongozi wa timu
zitakazoshiriki michuano ya Kombe la Kagame zikiwemo Simba, Yanga na Falcon
nchini Sudan, watalazimika kuvaa fulana zisizopitisha risasi kwa ajili ya
usalama.
Hayo
yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla
wakati akitoa msimamo mpya wa serikali juu ya ushiriki wa timu za Tanzania
katika michuano hiyo.
Awali,
Simba, Yanga na Falcon zilikuwa kwenye uwezekano wa kutoshiriki kwa sababu za
kiusalana hasa katika Jimbo la Darfur ambalo ni kiini cha machafuko nchini
humo.
Makalla
alisema baada ya Serikali ya Sudan kuihakikishia Tanzania usalama, timu hizo
zitashiriki lakini wachezaji na viongozi wake watavalia fulana hizo
zisizopitisha risasi.
Makalla
alisema jana kuwa Serikali ya Sudan pia imethibitisha kwa barua kwamba
itawapokea wachezaji hao kuanzia Khartoum ambako timu hizo zitafikia na
kuwasafirisha kwa basi hadi miji ya Darfur na Kordofan.
Uamuzi
huo unakuja siku nne tu, tangu Makalla alitangazie Bunge kuwa, Tanzania
haitapeleka timu zake katika nchi hiyo kutokana na usalama mdogo, wakati
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM).
Makalla
alisema jana, awali walichukua msimamo huo wa kutokana na kutokuwa na
uthibitisho kutoka kwa nchi husika, badala yake Baraza la Vyama vya Soka Ukanda
wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ndilo limekuwa likitoa taarifa.
“Kwa
taarifa tulizozipata, mazingira ya kule hayakuwa salama na tulimtaka Leodegar
Tenga ambaye ni Mwenyekiti wa Cecafa, yeye kama Mtanzania mwenzetu, suala hili
anabebaje dhamana na pia tukamtaka atueleze, kwanini tunapata uthibitisho
kutoka CECAFA badala ya serikali. Hatimaye sasa serikali yenyewe ndiyo
imetuandikia barua,” alisema.
Juni
1, Waziri wa Mambo ya Nje,
Bernard Membe wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya wizara
yake, alisema anashangaa kuona Darfur ikipewa uenyeji wa michuano hiyo licha ya
kuwa na usalama mdogo.
Alisema
kwa mujibu wa sheria za kimataifa kwenye nchi zenye machafuko ili michuano kama
hiyo iweze kufanyika ni lazima sehemu husika wanakofikia wachezaji na maofisa
wengine, kuwe na magari maalumu ya kuzuia risasi (bullet proof) ya kuwabeba
kutoka uwanja wa ndege hadi sehemu wanakokwenda.
Membe
alisema wachezaji na viongozi wengine watakaokwenda Darfur, wanapaswa kupewa
fulana maalumu za kuzuia risasi, ambazo watapaswa kuzivaa wakati wote kwa ajili
ya usalama wao.
Aliongeza
kuwa mbali ya matatizo ya kiusalama, pia mji wa Darfur hauna hoteli zenye uwezo
wa kuwatosheleza wageni wote watakaokwenda kwa ajili ya michuano hiyo.
Waziri
Membe alihoji busara gani iliyotumiwa na CECAFA kuteua nchi hiyo kuwa mwenyeji
wa michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 18.
Wakati
Yanga ikishiriki michuano hiyo kama bingwa mtetezi, Simba imejitwalia tiketi ya
moja kwa moja kama mabingwa wa msimu uliopita, kama ilivyo kwa Falcon, ambayo
licha ya kushuka daraja msimu huu, itashiriki michuano hiyo.
Tangu
mwaka 2002, michuano hiyo imekuwa ikifanyika chini ya udhamini wa Rais wa
Rwanda, Paul Kagame, ambaye hutoa zawadi kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu.
0 comments:
Post a Comment