Saturday, 15 June 2013

AHUKUMIWA JELA KWA KUMZUIA JIRANI YAKE ASIPITE

  MWANAUME mmoja aliyekataa kumpisha jirani yake njiani na kutisha kumpiga, alitozwa faini ya Sh3,000 au asukumwe jela mwezi mmoja akishindwa kulipa faini hiyo.

Bw Martin Ng’ang’a alipata adhabu hiyo baada ya kukiri kwamba alikataa kuondoka barabarani kumpisha Bw Daniel Kibe Kihara kupita na kumwambia kwamba angempiga.

Mahakama iliambiwa kwamba alitenda kosa hilo mjini Ongata Rongai, tendo ambalo ni kuvuruga amani ya mlalamishi.

Kiongozi wa mashtaka Inspekta Mkuu John Kiilu aliambia mahakama kwamba Bw Kibe alikuwa akiendesha gari lake akielekea nyumbani mshtakiwa alipokataa kuondoka barabarani. Alipomwambia aondoke, alitisha kumpiga na kumwambia alikuwa mjinga.

Bw Kiilu alisema mlalamishi alipiga ripoti katika kambi ya chifu na mshtakiwa akakamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Ongata Rongai kisha akafunguliwa mashtaka.

Akililia mahakama, Ng’ang’a aliomba ahurumiwe akisema alikuwa mlevi alipotenda kosa hilo.

Alisema mlalamishi ni jirani yake wa muda mrefu na hakutaka ujirani wao uvurugike.

Lakini Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Bi Juma Osoro alimwambia ulevi haufai kuwa kisingizio cha kutenda makosa na kumtoza faini au afungwe jela mwezi mmoja.

Source:  SwahiliHub, Kenya

0 comments: