Taifa Stars inatupa karata yake ya pili
ugenini kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia kwa kesho (Juni 8 mwaka huu)
kuikabili Morocco (Lions of the Atlas) kwenye Uwanja wa Grand Stade hapa
Marrakech, Morocco.
Ilipoteza
ya kwanza ugenini dhidi ya Ivory Coast mwaka jana, na kushinda mbili mfululizo
nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco. Mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 3
usiku kwa saa za Morocco ni ya pili kwa Stars katika uwanja huo ambapo mwaka
juzi ilifungwa mabao 3-1.
Washabiki
wa Morocco wanaonekana kuikatia tama timu yao yenye pointi mbili tu nyuma ya
Ivory Coast inayoongoza kundi hilo la C ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na
Tanzania yenye sita. Huo ni mtazamo wa washabiki, lakini kwa upande wa timu
inaonekana imepania kujichomoa katika nafasi za chini.
Kwa
upande wa Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema timu yake imepania mechi hiyo,
lengo likiwa ni kuona inapata matokeo mazuri baada ya dakika 90 za mechi hiyo
itakayokuwa chini ya refa Daniel Frazier Bennett wa Afrika Kusini.
Amesema
timu yake itacheza kwa umakini na uangalifu kwa vile wanajua wapinzani wao
wakicheza mbele ya washabiki wao watakuwa katika shinikizo za kushinda, jambo
ambalo wamejiandaa kukabiliana nalo.
Kwa
upande wa maandalizi, Kim amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
na wadhamini wa timu hiyo Kilimanjaro Premium Lager wameiandaa vizuri kwani iko
kambini kwa wiki tatu sasa na kupata mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan
iliyochezwa wiki iliyopita nchini Ethiopia.
Stars
iliifunga Morocco mabao 3-1 zilipokutana Machi 24 mwaka huu jijini Dar es Salaa.
Lakini zilipokutana hapa Marrakech mara ya mwisho mwaka 2011, Morocco iliibuka
na ushindi wa mabao 3-1.
Kim
amesisitiza kuwa kikosi chake kimepania kufanya vizuri katika michuano hii ya
mchujo ya Kombe la Dunia, ha hiyo inathibitishwa na matokeo ya timu kadri
inavyoendelea kucheza mechi za mashindano.
“Moja
ya mipango yetu katika mechi hizi za Kombe la Dunia ni kushinda nyumbani, hilo
hadi sasa tumelifanya kwa asilimia 100. Lakini ili tukae vizuri zaidi tumekuja
hapa Morocco kwa lengo la kupata matokeo mazuri, ingawa tunajua mechi itakuwa
ngumi,” amesema kocha huyo raia wa Denmark.
Kwa
hapa Marrakech mechi hiyo imekuwa haizungumzwi mara kwa mara, na kubwa ni kuwa
Wamorocco wengi wanaamini kuwa timu yao ambayo hadi sasa ina pointi mbili haina
nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano hiyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Marrakech, Morocco
0 comments:
Post a Comment