Tuesday 2 September 2014

MAMA ATEKETWA KWA MOTO WA PETROLI ANGALA HAPA




MAMA mmoja mjane, Mwajuma Hamisi Lissu (42) ameteketea kwa moto baada ya nyumba aliyokuwa amelala eneo la Kibamba Hondogo A maarufu Miti Mirefu jijini Dar es Salaam, kulipuliwa kwa petroli usiku wa  Agosti 24, mwaka  huu.

Tukio hilo la kusikitisha inadaiwa linahusishwa  na ugomvi baada ya mama  huyo kuachana na ulokole na  kujiunga tena katika dini yake ya zamani ya Kiislamu.Akisimulia mazingira ya tukio hilo, mtoto wa pili wa mama huyo ambaye hivi sasa ni marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Charity Jikole alikuwa na haya ya kusema:

“Mama amelipuliwa na petroli. Baada ya moto huo kulipuka chumbani tulikuta nyavu za kwenye dirisha la chumba alicholala zimekatwa, tunaamini mlipuaji ndiye aliyekata nyavu hizo na kupitishia petroli.
 
“Mauaji haya siyo ya bahati mbaya bali yanatokana na mkono wa mtu kwani hata moto ulipokuwa unawaka harufu ya petroli ilikuwepo eneo hilo.

“Mkasa huu unatokana na ukweli kuwa mama yangu awali alikuwa Muislamu lakini kutokana na matatizo yake ya kiafya alishauriwa na baadhi ya watu kujiunga na maombi katika makanisa ya kilokole ili awe anaombewa tatizo la presha.
 
“Baada ya kushauriwa aliamua kujiunga na makanisa hayo ya kilokole akiamini kuwa angeweza kupona.

“Mama alikuwa ni mjane mwenye watoto watatu na baada ya kujiunga na walokole amekuwa akisali katika makanisa manne tofauti.

“Sisi kama familia tunawatuhumu walokole kwa  sababu hata baada ya moto  huo, baadhi yao hawakuja kusaidia kuuzima wala kutoa maji.

“Kwa kweli tulishangazwa na kitendo hicho na kuwaona ni watu wabaya sana kwetu.”
 
Hata hivyo, mtoto huyo alisema kifo cha mama yake kimekuja siku moja baada ya kufanyiwa sherehe ya kutoka katika dini ya kilokole na kurudi kwenye Uislamu.
 
Mchungaji aliyetajwa kwa jina la George Said ambaye anawaongoza walokole wa eneo hilo, alipohojiwa na waandishi wetu alikiri kusikia tuhuma hizo.

“Hata mimi nimesikia tuhuma hizo lakini si za kweli hata kidogo na mpaka sasa sijahojiwa na mtu yeyote au hata polisi kuhusiana na tatizo hilo,” alisema  mchungaji huyo.
 
 

0 comments: