Tuesday 5 August 2014

HOT NEWS YANGA SC YAENGULIWA KOMBE LA KAGAME, AZAM WACHUKUA NAFASI KIGALI

 



BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeiengua Yanga SC katika michuano ya Kombe la Kagame na nafasi hiyo kupewa Azam FC, zote zaTanzania.
Yanga SC imeenguliwa kwa sababu moja tu kubwa, kushindwa kuthibitisha kupeleka kikosi cha kwanza pamoja na kocha Mkuu, Marcio Maximo kwa mujibu wa kanuni za mashindano.
Yanga SC ilitakiwa hadi jana jioni kuwa imethibitisha na kutuma kikosi, lakini haikufanya hivyo na CECAFA ikawasiliana na TFF kuwaambia wapeleke timu nyingine iliyo tayari, ndipo zali likawaangukia Azam FC.
Yanga SC ilitaka kupeleka kikosi cha vijana kwenye nashindano hayo, jambo ambalo CECAFA waliwakatalia wakiwaambia hiyo si michuano ya watoto.
Azam FC, mabingwa wa Tanzania Bara, sasa wanaingia Kundi A katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame ya 40 pamoja na wenyeji, Rayon Sport, Coffee ya Ethiopia, Atlabara ya Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar.
Kundi B lina timu za APR ya Rwanda, KCC ya Uganda, Flambeau de L’Est ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na Telecom ya Djibouti wakati Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya Burundi, El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.
Timu 14 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo kuanzia Agosti 8 hadi 24 mwaka huu- jumla ya mechi 34 zikichezwa katika viwanja vya Amahoro na Nyamirambo, Kigali
Rais Paul Kagame wa Rwanda ndiye mlezi wa mashindano haya ambaye hutoa dola za Kimarekani 60,000 kila mwaka kwa ajili ya zawadi.
Wizara ya Michezo ya Rwanda na mashirika mengine yatadhamini michuano hiyo, itakayokwenda sambamba na maazimisho ya miaka 20 ya mauwaji ya kimbau.
Televisheni ya kulipia ya Supersport ya Afrika Kusini ambao ni maswahiba wa muda mrefu wa CECAFA, ni miongoni mwa wadhamini pia na wataonyesha mechi zote za michuano hiyo moja kwa moja. 
Kwa kuwa Azam imechukua nafasi ya Yanga, sasa itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Rayon Sport Uwanja wa Amahoro Agosti 8, mwaka huu, mchezo ambao utatanguliwan na mechi kati ya 
KMKM ya Zanzibar na Atlabara ya Sudan Kusini. 
Azam FC itarudi tena dimbani, Agosti 10 kumenyana na jirani zao KMKM, kabla ya kucheza na Atlabara Agosti 12 na kukamilisha mechi za kundi lake, kwa kumenyana na Coffee ya Ethiopia Agosti 16.
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM

0 comments: