Sunday, 18 May 2014

MAGEUZI YA RAIS ABDELAZIZI BOUTEFLIKA WA ALGERIA

 

    Sambamba na kuanza kwa duru ya nne ya uongozi wa Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria, katika hatua ya kwanza ya marekebisho, rais huyo ametaka kupunguzwa mihula ya utawala wa urais na kuwa mihula miwili, sanjari na kukabidhiwa mamlaka makubwa kwa waziri mkuu wa nchi. Algeria ni nchi kubwa ya kaskazini magharibi mwa Afrika, ambayo ina jamii ya watu milioni 37. Uchaguzi wa kwanza huru wa rais nchini humo ulifanyika mwaka 1999. Jina la Abdelaziz Bouteflika lilivuma sana na kuwavutia raia wengi wa nchi hiyo katika uchaguzi wa mwaka huo na hivyo kumpa idhini ya kuiongoza Algeria. Mwaka 2004 Rais Abdelaziz Bouteflika alishinda uchaguzi mwingine wa rais na kuchaguliwa tena kuwa rais wa taifa hilo. Kwa mujibu wa katiba ya wakati huo, rais alitakiwa kusalia madarakani kwa kipindi cha mihula isiyozidi miwili ya miaka mitanomitano. Hata hivyo mwaka 2008 rais huyo wa Algeria aliifanyia marekebisho katiba hiyo na kuongeza muhula wa urais kutoka mihula miwili ya miaka mitanomitano na kuwa mihula kadhaa isiyokuwa na kikomo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Rais Bouteflika akachaguliwa tena kwa awamu ya tatu mwaka 2009. Kama hiyo haitoshi akiwa na umri wa miaka 77rais huyo alichaguliwa tena mwaka huu, kwa kipindi kingine cha muhula wa nne mtawalia kuiongoza nchi hiyo ya kaskazini magharibi mwa Afrika. Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa sana na wananchi dhidi ya Bouteflika ni suala la uongozi usio na kikomo jambo ambalo limekita mizizi katika nchi nyingi za Kiarabu. Aidha suala hilo ndilo limekuwa msingi wa kuibuka upinzani mkubwa dhidi ya serikali nchini Algeria katika miaka ya hivi karibuni. Licha ya serikali ya Algiers kufanya juhudi kubwa za kufunika ukweli wa mambo na kutangaza kuwa, chanzo kikuu cha kuibuka upinzani, maandamano na malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali katika miaka kadhaa ya hivi karibunii yakiwemo maandamano ya mwaka 2011, eti kilitokana na sababu za kiuchumi na ughali wa maisha, lakini ukweli wa mambo unaonyesha kwamba, maandamano na upinzani huo ulikuwa wa kulalamikia mfumo wa utawala usio na muda maalumu nchini. Wapinzani wa Algeria wamekuwa wakitaka kufanyiwa marekebisho ya kisiasa na kupatikana mabadiliko katika mfumo wa utawala wa nchi yao. Ni kwa ajili hiyo ndio katika kampeni za uchaguzi wa urais uliomalizika hapo tarehe 17 mwezi Aprili na uliowashririkisha wagombea sita wa urais, Rais Bouteflika akaahidi kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ili uwezekane kupatikana mfumo wa uongozi wa demokrasia shirikishi. Katika uchaguzi huo Rais Bouteflika alishinda kwa kupata asilimia 53. 18 ya kura. Tarehe 28 mwezi jana na katika sherehe za kuapishwa rais huyo alitangaza kuwa, angeamuru haraka kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi kuelekea katiba ya maridhiano. Inaonekana kuwa, pendekezo la Rais Abdelaziz Bouteflika la kubadili kipengee cha 74 cha katiba ya Algeria na kukirejesha katika hali yake ya awali kabla ya kuifanyia marekebisho katiba hiyo hapo mwaka 2008, lina lengo la kuzuia upinzani mpya wa wananchi wa taifa hilo. Hata hivyo tunatakiwa kusubiri kuona iwapo wapinzani wa serikali ya Algiers watakubaliana na pendekezo hilo la Bouteflika au ndio kwanza wataitaja kuwa hatua iliyochelewa?

    0 comments: