Monday 9 November 2015

Ushauri Kwa Rais Dr John Magufuli Kuhusu Kutumia Lugha ya Kiswahili Ndani na Nje ya Nchi Kwenye Mikutano

 
Ili kuipa hadhi na kuitangaza lugha yetu ya taifa, nashauri rais wetu mpya atumie Kiswahili katika shughuli zote rasmi za kitaifa na kimataifa. Cha msingi ni kuwa na wakalimani mahiri katika shughuli za kimataifa. Hii itainua hadhi na heshima ya nchi yetu badala ya kuendelea kuthamini lugha za kigeni. Tumekuwa watumwa mno wa lugha ya kiingereza mpaka kufikia hatua kudhani kuwa mtu anayeongea kiingereza vizuri ndiye aliye elimika wakati si kweli. Elimu ni uwezo siyo kuongea kiingereza. 

Hiki kiingereza cha "izi, wozi, wea, kongrugesheni, ameizingi, wati?, yu no, no problemu hakitusaidii kitu. Na kwa ujinga wetu tunafundishana kwa lugha tusiyoijua vizuri matokeo yake watoto wanafeli halafu tunawaona wajinga kumbe sera zetu ndio mbovu. Wachina, wakorea, wajerumani, wareno, wafaransa mbona wanatumia lugha zao na wanapiga hatua kubwa sana katika uchumi na sayansi. Sisi na kiingereza chetu cha kuombea maji tumefika wapi zaidi ya kutudhalilisha?

Maoni yangu haya hayana maana kuwa sitambui uwezo mkubwa wa kiingereza alio nao dr. Nataka aendeleze pale mwenzake alipoachia mwenzake, kwani alianza kwa kuhutubia kwa kiswahili kwenye mkutano wa AU lakini baadaye akaacha. Mimi nashauri Dr. sasa ajikite pamoja na mambo mengi kuitangaza lugha ya kiswahili kimataifa kwa yeye mwenyewe kuitumia badala ya kiingereza. Huwa naona viongozi wa nchi nyingine kama za kiarabu pamoja na kuwa wanajua kiingereza lakini utakuta wanazaunguza kiarabu na kisha wasiojua kutafsiriwa. Wakalimani sasa hivi tunao wengi, ni vizuri wakatumika vizuri kuikuza lugha yetu ya taifa. 

Ukweli ni kuwa unapotumia lugha mama au lugha ya taifa una kuwa na uhuru na uwezo mkubwa sana wa kujieleza na kuelezea kuliko unapotumia lugha za kigeni. Kwa watanzania wengi lugha yetu ya mama ni kiswahili.

0 comments: