Wednesday, 23 October 2013

MERRY MWANJELWA :ASEMA TUACHE CHIKI NA MALUMBANO TUPIGE KAZI

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Mbeya, Dk.Mary Mwanjelwa

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Mbeya, Dk. Mary Mwanjelwa amewata wakazi wa jiji la Mbeya kuwapuuza watu wanaotumia mbinu chafu za kuwachonganisha viongozi wa kisiasa kwa maslahi yao binafsi kwani kufanya hivyo kunachelewesha kupatikana kwa maendeleo katika jiji hilo.

Kauli ya Dk. Mwanjelwa imekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari   kueleza kuwa alimsema vibaya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Mr. Sugu wakati wa mikutano ya hadhara ya ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba mkoani humo.


Dk. Mwanjelwa alisema wananchi wa jiji la Mbeya lazima watambue kuwa viongozi wa kisiasa waliowachagua wanajukumu moja muhimu la kuwaletea maendeleo, hivyo suala la baadhi ya watu kutumia mbinu za kuwachonganisha lisipewe nafasi kwa mustakabali wa maendeleo ya jiji hilo.


“Mheshimiwa Joseph Mbilinyi au Sugu ni mbunge mwenzangu, na ninamheshimu kama kiongozi mwenzangu hata kama itikadi zetu ni tofauti, Mbeya yetu ina changamoto za maendeleo ambazo sisi wanasiasa tunatakiwa kukabiliana nazo ili wananchi wanufaike na uwepo wetu,” alisema Dk. Mwanjelwa.


Katika hatua nyingine, Mbunge huyo, akiwa katika ziara yake jijini Mbeya alitoa wito kwa Watanzania kutumia dawa za asili zisizo na kemikali ili waweze kuwa na afya njema na kuishi maisha marefu.


Akifungua maonyesho ya wajasiriamali yaliyoshirikisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda jijini Mbeya juzi, Dk. Mwanjelwa alisema matumizi ya dawa za asili yana faida kubwa ikiwamo watumiaji kuwa na maisha marefu zaidi na mfano mzuri ni wazee ambao wengi wao zamani walitibiwa kwa dawa hizo tofauti na sasa.


Aidha, aliwashauri wajasiriamali wa Tanzania kuongeza ubora wa usindikaji bidhaa ili kumudu soko la ushindani hasa na nchi ya Kenya ambayo alisema wajasiriamali wake wanapata malighafi kutoka Tanzania lakini wanakuwa na soko kubwa kutokana na usindikaji wao.

 “Nitoe wito kwa vijana na wanawake mkoani Mbeya kuunda vikundi na kuvisajili kisha njooni ofisini kwangu tuwasaidiane’’ alisema Mbunge huyo.

Kwa upande wa waandaaji wa maonyesho hayo ya wajasiriamali, kampuni ya MTF, walisema licha ya maonyesho hayo kufanyika mkoani Mbeya, lakini wajasiriamali waliojitokeza kwa wingi ni kutoka nje ya mkoa huo.


Alisema lengo la maonyesho hayo ni kukuza ujasiriamali na kutangaza muziki asili zikiwamo ngoma kwa ajili ya kudumisha utamaduni wa Mtanzania.


 By Thobias Mwanakatwe 
source nipashe gazeti
 

0 comments: