Wednesday 23 October 2013

ASKARI WA TANAPA WADAIWA KUUA MTU MMOJA TARIME MKOANI MARA NI

 
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa)

Mtu  mmoja mkazi wa kijiji cha Mrito Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Peter Maseya ameuawa na watu wanaodaiwa kuwa  askari wa  Mamlaka ya  Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na mwili wake kutelekezwa kituo cha Lamai.

Kufuatia tukio hilo, ndugu wa marehemu wamegoma kuuchukua mwili kwa zaidi ya siku saba sasa wakishinikiza hadi ufanyiwe uchunguzi kujua sababu za kifo cha ndugu yao.

Meneja Uhusiano wa Tanapa, Pascal Shalutete, alipotafutwa katika simu yake hakupatikana.

Chacha Masero mmoja wa ndugu wa marehemu alisema Oktoba 13, mwaka huu askari wa Tanapa walifika nyumba kwa Maseya (marehemu) saa 8:00 usiku na kumkamata yeye na watoto wake wawili ambao ni Mwita, Maseya na mchunga ng’ombe.


Baada ya kumkamata walianza kumhoji na kumtaka aonyeshe ilipo silaha anayodaiwa kuuziwa na mtu mmoja aliyekamatwa waliokuwa wakimshikilia akihusishwa na masuala ya ujangili.


Alisema askari hao walimchukua hadi Tarime mjini ambako walianza kumpiga, lakini alikataa kwamba hana silaha yeyote aliyouziwa na mtu.


Aliongeza kuwa baadaye askari hao walimpigia simu mke wa marehemu wakimtaka apeleke silaha ya mume wake, lakini aliwaeleza kuwa mume wake hana silaha yeyote.

Baadaye watoto waliachiwa huru, lakini baba yao  (Maseya) alibakia akiendelea kupewa kipigo na inadaiwa walimpeleka kusikojulikana.

Oktoba 15, mwaka huu, ndugu walianza kumtafuta ndugu yao na kutoa taarifa wilayani na kuonana na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya  (OCCID), Fadhir Luwoga.

Siku iliyofuata (Oktoba 16) walipata taarifa kuwa Maseya amefariki na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya DDH Mgumu.

Masero alisema baada ya kupata taarifa hizo walikubaliana kuwa wasiuchukue mwili wa marehemu hadi kufanyike uchunguzi wa kina kujua sababu za kifo chake.


Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Tarime, Luwoga, alithibitisha  kutokea kwa taarifa hizo na kwamba wamekubaliana na ndugu za marehemu ambao jana waliuchukua mwili wa marehemu kwa maziko.

By Thobias Mwanakatwe 
SOURCE: NIPASHE

0 comments: