BAADA ya
kutowatumia wachezaji wake wanne wa kikosi cha kwanza katika mchezo wa jana
dhidi ya Rhino Rangers, Kocha wa Yanga, Ernie Brandts amesema amelazimika kuwapumzisha
wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza kutokana na uchovu.
Katika mchezo
dhidi ya Rhino Rangers Jumatano iliyopita, Brandts hakuwatumia wachezaji Didier
Kavumbagu, Athuman Idd ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Ali Mustapha
‘Barthez’, lakini kikosi kilichoanza kiliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Tofauti ya
Cannavaro na Barthez, Chuji na Kavumbagu wenyewe waliwekwa benchi lakini
hawakuweza kupewa nafasi ya kucheza katika mchezo huo ulionekana kikosi cha
Yanga kilichoanza kinaweza kuhimili vishindo vya Rhino.
Mara baada ya
mchezo huo, Brandts aliuambia mtandao huu kwamba, hakuwachezesha wachezaji hao kutokana
na kutumika katika mechi nyingi za Yanga hivyo aliamua kuwapumzisha ili
watumike katika mechi zinazofuata.
“Ni kweli
sikuwapanga Chuji, Cannavaro na wengine ambao mmezoea kuwaona kikosi cha kwanza
kutokana na kuwa wametumika sana hivyo niliamua kuwapumzisha ili niweze
kuwatumia katika michezo ijayo na sikuwa na maana nyingine nje ya hiyo.
“Yanga imesajili
zaidi ya wachezaji 25, hivyo kutowatumia wachezaji fulani wa kikosi cha kwanza,
haina maana kwamba wapo katika adhabu au kuna jambo tofauti lililotokea naomba
nieleweke hivyo, mtawaona katika mechi zijazo hao wachezaji wala msiwe na
shaka,” alisema Brandts.
Kikosi cha jana
cha Yanga kiliwakilishwa na Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, David
Luhende, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Rajab Zahir, Simon Msuva, Frank Domayo, Hamisi
Kiiza, Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima.
Katika kikosi
hicho, Brandts aliwafanyia mabadiliko Msuva na Luhende ambao nafasi zao
zilichukuliwa na Oscar Joshua na Nizar Khalfan.
Yanga ambayo
sasa ina pointi 19 katika mechi 10 ilizocheza, Jumanne ijayo inatarajiwa
kucheza na Mgambo JKT katika muendelezo wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam. Yanga inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo yenye
timu 14.
0 comments:
Post a Comment