Wednesday, 21 May 2014

POPPE ALETA NEEMA SIMBA SC KWA SHARTI MOJA TU

, YEYE NA WAFADHILI WENGINE WATANO WATAMWAGA NOTI ‘BWENA’ MSIMBAZI


MWENYEKITI wa Friends Of Simba (F.O.S.), Zacharia Hans Poppe amewaambia wanachama wa Simba SC wahakikishe wanachagua viongozi wazuri katika uchaguzi wa klabu hiyo Juni 29, mwaka huu, vinginevyo hatakuwa tayari kushirikia na viongozi wasiofaa. “Na siyo mimi tu, kuna wafadhili wengine sita nimewapata ambao wamekubali kuisaidia Simba SC, iwapo tu uchaguzi wa mwezi ujao utazalisha viongozi bora wenye kuaminika,” amesema Hans Poppe akizungumza na BIN ZUBEIRY leo. Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba baada ya miaka minne ya kuvumilia kufanya chini ya uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage, hatakuwa tayari kupoteza muda na fedha zake kwa mara nyingine kwa kuwasaidia viongozi wengine bomu iwapo watachaguliwa.
Chagueni watu makini; Zacharia Hans Poppe ametoa nasaha zake kuelekea uchaguzi Mkuu Simba SC
“Tunapoteza muda wetu, tunajitolea kwa hali na mali kuisaidia Simba SC, lakini inapotokea klabu inakuwa na viongozi wa ovyo, yote hayo yanakuwa kazi bure. Sasa napenda nichukue fursa hii kuwaasa, wanachama wenzangu wa Simba SC, wawe makini safari hii kuhakikisha wanachagua viongozi bora, ili tuweze kurudisha zama za heshima ndani ya klabu yetu,”amesema. Poppe amesema kwamba kuanzia msimu ujao ushindani utaongezeka katika soka ya Tanzania kutokana na timu nyingi kuja juu, hivyo Simba SC inapaswa kuwa imara sana chini ya viongozi bora ili kuweza kuhimili vishindo vya ushindani. “Hatutakiwi kufanya mzaha hata kidogo, tuweke mbele maslahi ya Simba SC na wote tuamue kwa manufaa ya Simba SC, tuonyeshe mapenzi yetu ya dhati kwa klabu kwa kuchagua viongozi bora, watakaoirudishia klabu hadhi yake,”amesema.  Poppe amewataka Simba SC watumie kura zao vizuri kwa kuchagua viongozi makini kuanzia nafasi za Ujumbe, Makamu wa Rais na Rais ili kuhakikisha klabu inakuwa katika mikono salama. “Achaguliwe mtu ambaye ana sapoti, anakubalika, ana historia na Simba SC, huko nyuma amewahi kuisaidia timu, siyo mtu ambaye anaibuka tu kuja kuomba uongozi, wakati hana rekodi za kusaidia timu. Lazima sana tuwe makini na tuwatathmini watu wanaokuja kutuomba uongozi, historia zao, siyo watu wa migogoro, hawana kashfa za ubadhirifu, wanashirikiana vizuri na wenzao na wana mapenzi ya dhati na Simba,”amesema Poppe. Kwa sasa Poppe mbali na kuwa Mwenyekiti wa F.O.S., pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo chini ya uongozi wa sasa wa Alhaj Rage unaomaliza muda wake. Poppe amekuwa mhimili muhimu mno ndani ya Simba SC kwa zaidi ya miaka mitano sasa akiisaidia kwa hali na mali klabu hiyo na wazi iwapo atarudisha mkono wake nyuma, klabu hiyo itayumba.
 
 Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam 

0 comments: