Dodoma. Vyama vya CUF na Chadema vimekubali kuombana radhi ili
mgogoro baina yao uishe baada ya misimamo ya pande zote kuvunja kikao
cha Bunge mara mbili, juzi.
Kutokana na maridhiano hayo, Bunge leo litaendelea
na mjadala wa makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na
Uhusiano wa Kimataifa, baada ya kukwamishwa mara mbili na mzozo huo.
Mzozo huo ulizuka baada ya hotuba iliyoandaliwa na
Chadema na kusomwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa wizara
hiyo, Ezekiel Wenje kudai kuwa CUF inafuata itikadi za Kiliberali ambazo
miongoni mwa misingi yake mikuu ni kupigania haki za ndoa za jinsia
moja yaani ‘usagaji’ na ‘ushoga’.
Vyama hivyo vyote viliombana radhi bungeni ili
kumaliza mzozo huo, baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuamuru
pande zote kufanya hivyo kulingana na ushauri wa Kamati ya Maadili ya
Bunge.
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe aliomba radhi kwa upande wa Chadema, wakati upande wa CUF aliomba
Mnadhimu Mkuu wa chama hicho Bungeni, Rashid ally Abdalah.
Pamoja na maombi hayo ya msamaha, pande zote
ziliendelea kusimamia misimamo yao, lakini wakasema wanazingatia
masilahi ya taifa kwa kuombana radhi ili Bunge liendelee kujadili bajeti
ya Wizara ya Mambo ya Nje.
Kuhusu kuihusisha CUF na sera zilizotajwa na
kuleta tafrani, Mbowe alisema: “Yapo mengi ya (wabunge) kuyajadili. Hili
(la ushoga na usagaji) siyo muhimu. Yapo mengi yenye masilahi kwa
taifa. Bunge limeahirishwa pasipo sababu ya msingi,” alisema Mbowe na
kuomba radhi.
Abdalah alikiri kuwa kauli ya Chadema ilizua
mtafaruku na hasira kwa wabunge wa Chama chake na hata kujikuta
wakifanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu.
“Damu ilichemka na kusababisha kutoa maneno ambayo hayafai Bungeni. Naomba radhi kwa hayo,” alisema Abdalah.
Kuomba radhi huko kulitokana na Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Maadili ya Bunge, John Chiligati kueleza kuwa baada ya
kuzungumza na pande zote pamoja na kufuata ushauri wa wabunge mbalimbali
walibaini pande zote zina makosa.
Chiligati alisema katika mahojiano, CUF ilikiri
kuwa inafuata sera za Kiliberali lakini siyo zote ikiwamo hiyo ya ushoga
na usagaji, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania haikubaliani na tabia ya
namna hiyo.
Kwa sababu hiyo, Chiligati alisema Chadema itaomba
radhi baada ya kubainika kufanya makosa mawili wakati CUF itaomba radhi
kwa vipengele vya makosa manne.
0 comments:
Post a Comment