Sunday, 2 June 2013

UHAMIAJI WALIOSHUGHULIKIA SUALA LA KABENDERA WACHUKULIWE HATUA

KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Emmanuel Nchimbi kuchunguza tukio la kusumbuliwa kwa wazazi wa mwandishi wa habari Erick Kabendera na maofisa Uhamiaji imependekeza maofisa hao wachukuliwe hatua stahiki za kinidhamu kwani walikiuka taratibu za kazi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Augustine Shio akisoma taarifa ya kamati hiyo jana mbele ya waandishi wa habari, alisema maofisa Uhamiaji waliochunguza uraia wa Erick na wazazi wake hawakuwa makini katika kazi yao.

Shio alisema kitendo cha kukosa umakini kilisababisha malalamiko kutoka familia ya Erick, wazazi wake pamoja na vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa uraia wa Erick, baba yake mzazi Nolosco Kabendera na mama yake Verdiana Mujwahuzi haubishaniwi kuwa wote ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa.

Lakini kamati hiyo imejiridhisha kwamba zipo kasoro za msingi za jina zilizobainika katika mchakato wa maombi ya pasipoti ya Erick iliyotolewa mwaka 2006 ambazo zilisababisha Idara ya Uhamiaji kufanya uchunguzi ili kuthibitisha taarifa za maombi hususani uraia wa mwombaji.

“Pia tumebaini kwamba Reginald Mengi hajahusika kwa namna yoyote na mchakato wa uchunguzi wa uraia wa Erick Kabendera na kuhojiwa kwa wazazi wake na Idara ya Uhamiaji,” alisema Shio ambaye ni Mkurugenzi wa Malalamiko katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Nchimbi aliunda kamati hiyo ya watu watatu Machi mwaka huu baada ya kuombwa na Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Idara ya Habari (Maelezo) na Jukwaa la Wahariri kuchunguza na kutafuta suluhisho la kuwepo matukio kadhaa ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari hapa nchini.

Katika mkutano wake na vyombo hivyo, mambo mbalimbali yaliwasilishwa lakini tukio moja la kusumbuliwa kwa wazazi wa Erick Kabendera kwa madai kuwa si raia wa Tanzania liliombwa lichunguzwe kwa maelezo kuwa kuna taarifa zisizotiliwa shaka na za kuamini kwamba watumishi wa Uhamiaji waliotumika walilipwa fedha ambazo hazikutoka katika mfumo rasmi wa Serikali bali zilitolewa na mtu mmoja zikapitia kwa ofisa wa Ikulu kwenda Uhamiaji.

Licha ya Moat, wengine ambao walilalamikia suala hilo ni waandishi wasio na mipaka pamoja na Erick mwenyewe ambao kwa nyakati tofauti waliandika barua kwenda kwa Waziri kulalamikia hatua hiyo ya Uhamiaji.

Barua hizo zilionesha kumhusisha Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi na tukio hilo hasa baada ya Erick kutoa ushahidi katika shauri la Mengi dhidi ya Sarah Hermitage katika Mahakama Kuu London, Uingereza.

Kamati hiyo pamoja na Shio, wengine walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni Mligo Mussa kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na Felix Wandwe mjumbe kutoka ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU).

---
Imenukuliwa kutoka HabariLeo


0 comments: