Sunday, 2 June 2013

MTOTO ATEKELEZWA NA MAMA YAKE BAA

 

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa mkazi wa wilayani Tarime, mkoani Mara, amemtelekeza mtoto wake kwenye baa mjini Bunda na kutokomea kusikojulikana.
Tukio hilo lililothibitishwa na jeshi la polisi, limetokea juzi jioni, katika baa moja iliyoko mjini Bunda, baada ya mwanamke huyo kufika katika eneo hilo na kumnunulia mtoto wake soda na andazi na kisha kuondoka akimwacha motto huyo.
Imeelezwa kuwa mwanamke huyo alimwacha mtoto wake huyo wa jinsi ya kike, ajulikanaye kwa jina la Lusia Mwita, anayekadiliwa kuwa na umri wa kati ya miaka mitano hadi sita, pamoja na mfuko wa wa nailoni uliokuwa na nguo za mtoto huyo.
Habari zaidi zinasema baada ya mtoto huyo kutelekezwa alianza kutangatanga, na ndipo akaokotwa kwenye uchochoro na mwanamke mmoja, ajulikanaye kwa jina la Pendo Joseph, mkazi wa mtaa wa Kabarimu mjini Bunda, ambaye alimpeleka kwenye kituo cha polisi.
Polisi wamesema kuwa baada ya mwanamke huyo kutoa maelezo yake, aliruhusiwa kuondoka na mtoto huyo, ambapo sasa anaishi naye akisubiri wazazi wake waweze kumchukuwa.
Akizungumza kwa taabu mtoto huyo amesema kuwa walipanda ndani ya basi kutoka Tarime, ambapo mama yake alimwambia kwamba wanakwenda kwa babu yake mjini Bunda, na baada ya kufika kwenye eneo hilo mama yake alimwacha na kwenda kusikojulikana.


Na Ahmed Makongo, Bunda

0 comments: