Wito
umetolewa kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan wazazi wenye
watoto walio na umri chini ya miaka 5 kuhakikisha kuwa wanashiriki
kikamilifu katika zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A na dawa za
Minyoo kwa kuwapeleka watoto wao katika vituo mbalimbali vya afya ili
waweze kupatiwa dawa hizo kabla ya terehe 20 mwezi huu.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki ametoa wito huo leo
jijini Dar es salaam kufuatia zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A na
dawa za minyoo kwa vituo vyote vya kutolea huduma vya Serikali,
binafsi na mashirika ya dini vilivyoainishwa katika manispaa za Ilala,
Temeke na Kinondoni kuelekea mwisho.
Amesema
zoezi hilo lililoanza tarehe 7 mwezi huu ni sehemu ya utekelezaji wa
mkakati wa Lishe wa Taifa uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka
2013 kwa lengo la kuongeza kasi ya uwajibikaji katika kuongeza hali ya
lishe nchini.
“Zoezi
hili sio geni kwani ni utaratibu ambao sote tunaufahamu kuwa Serikali
yetu kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau
wa Afya huendesha zoezi huendesha zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini
A na dawa za Minyoo kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5 nchi
nzima kila mwaka”
Amesema
zoezi la utoaji wa dawa hizo ni muhimu kutokana na miili ya watoto hao
kuwa katika mahitaji makubwa ya vitamin A kutokana na mchango wake
katika ukuaji wa miili na akili kwa kuimarisha uwezo wa kinga zao dhidi
ya magonjwa pamoja na kuimarisha uwezo wa macho.
Kwa
upande wake mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Grace Magembe
akizungumza kuhusu zoezi hilo ambalo linafikia kilele chake tarehe 20
mwezi huu amesema kuwa ni vema jamii ikawa na mwitikio chanya kwa zoezi
hili kutokana na umuhimu wake kwa watoto walio na umri chini ya miaka
5.
Amesema
kuwa zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A huokoa maisha ya watoto
kwani huwalinda na dhidi ya maradhi hatari kama vile Kuharisha, Surua na
maradhi ya mfumo wa hewa.
“Kila
mzazi anatamani kumuona mtoto wake anakua akiwa na afya njema, watoto
wenye upungufu wa Vitamini A wapo katika hatari ya kuugua maradhi,kupata
upofu na hata kupoteza maisha” Amesisitiza.
Aidha,
amesisitiza kuwa dawa zinazotolewa katika zoezi hilo ni salama kwani
tayari zimepitishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na
kuthibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) na Shirika la
Afya Duniani (WHO).
“Nawasihi wananchi mjitokeze kwa wingi katika zoezi hili kwa siku zilizobaki kwa kuwa zoezi hili tunaloliendesha ni salama”
0 comments:
Post a Comment