Nyota ya
Tanzania katika sanaa imepata mwangaza na msukumo mpya baada ya msanii
wake mahiri, Naseeb Abdul au Diamond kuteuliwa kuwania tuzo maarufu za
BET zitakazofanyika baadaye mwaka huu kule Marekani.
Tuzo hizo
ambazo zilianza rasmi 2001, zinalenga katika kuwaunganisha wasanii wote
wenye asili ya Afrika nchini Marekani na tangu kuanzishwa kwake
zimekuwa zikiwashirikisha wasanii mbalimbali kutoka sehemu nyingi
duniani ikiwamo nchi za Afrika
Uteuzi huu wa Diamond ambaye anashiriki kwa mara ya kwanza ni sifa kwa Tanzania na pia ukanda wa Afrika Mashariki kwa jumla.
Tunapenda
kumpongeza msanii huyu kijana ambaye mwezi huu pia ametwaa tuzo saba
kwenye tuzo za Kilimanjaro, jambo ambalo linaifanya nchi yetu kuingiza
mshindani halisi.
Hata
hivyo, Diamond ambaye anashiriki pia tuzo za MTV pamoja na zile za Kora,
anachuana na wakali wengine kutoka barani Afrika kama vile, Mafikizolo
(Afrika Kusini), Davido, Tiwa Savage (Nigeria) na wasanii wengine kadhaa
kutoka Ghana na Togo.
Tunatambua
kuwa huu ni mtihani mkubwa si kwake kama Diamond, bali kwa Tanzania na
Afrika Mashariki kwa jumla, lakini tunatambua kuwa ushindi wake
unamtegemea kila mmoja wetu.
Hata
hivyo, imekuwa ni kama bahati mbaya kwetu sisi Watanzania kwani hatuna
utamaduni wa kuwapigia kura washiriki wetu kwenye matukio mbalimbali ya
kimataifa, jambo ambalo hatuna budi kulibadili sasa ili kumwezesha
Diamond awe mshindi. Tumeona, huko nyuma kwa mfano kwenye shindano la
Big Brother Africa, tuzo za filamu bora ya Kiafrika kwa Kiswahili
zilizofanyika Nigeria mwaka huu ambako wasanii wetu waliangushwa si kwa
kukosa sifa, vigezo bali kwa kukosa kura.
Hivyo,
tunasema wakati ukifika, kushiriki kwetu na kupiga kura zetu kwa njia ya
mtandao, bila shaka tutakuwa tumemwezesha kijana wetu huyu kushiriki,
kushindana na pengine kufanya vizuri mwaka huu kwenye tuzo hizo.
Tuna
imani kwamba vijana ambao ni wengi na ambao siku hizi wanaishi kwenye
mitandao ya kijamii bila shaka watakuwa mabalozi wazuri wa kumwezesha
Diamond kuwa mshindi na pia balozi mzuri wa nchi yetu huko Marekani.
Tunadhani,
Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na hata balozi zetu
zilizoko nje pia zitashiriki katika kuhakikisha kuwa Diamond anaibuka
mshindi kwani hakuna kisichowezekana chini ya jua na washindi siku zote
hutengenezwa.
Inawezekana
hata sisi kumtengeneza mshindi etu, ambaye ni Diamond kwani yeye ndiye
pekee kutoka Tanzania, ingawa ukanda wa Afrika Mashariki unaye pia
Lupita Nyong'o kutoka Kenya ambaye mapema mwaka huu alishinda tuzo za
Oscars kwenye uigizaji.
Tunapenda
kutoa ushauri kwa wasanii wengine wa fani mbalimbali waige kutoka
kwenye mafanikio ya mwenzao huyu na kuamini kuwa inawezekana kuwa
mshindi, hasa kwa kufanya kazi kwa nidhamu, kujiamini na kujituma..
MAKALA HII IMEANDKWA NA(Martha Magessa)
0 comments:
Post a Comment