Monday, 3 June 2013

UHABA WA VIFAA VYA SABABISHA WAGONJWA WALALA CHINI MKOANI TANGA

  


HOSPITALI ya wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga inakabiliwa na Uhaba wa majengo ya wodi ya Mama na Mtoto hali inambayo imesababisha wagonjwa kulala zaidi wawili katika kitanda kimoja.

Pia hospitali hiyo inakabiliwa na upungu mkubwa wa Mashuka na malanketi kwa ajili ya kujifunika wagonjwa hali inawalazimu  wagonjwa hao  kujifunika mashuka yakiwa hayajakauka kutokana na uchache wa mashuka yaliyopo.

Hayo yamebainishwa na, Ofisa tabibu  mkuu wa Hospitali hiyo (Medical officer incharge) Dk Gasto Stephano  wakati wa akipokea msaada wa mashuka yaliyotolewa na umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) tawi la chuo kikuu cha kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), na kusema kuwa, hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa wodi ya mama na mtoto kutokana na majengo yake kujengwa tangu mwaka 1961.

Dk. Stefano alisema kuwa majengo yaliyoko kwa sasa hayakidhi mahitaji ya wagonjwa kulingana na idadi ya wagonjwa walioko kwa sasa kuongezeka na kuzidi kiwango kilicho kasimiwa wakati wa ujenzi wa hospitali, hali inayowalazimu  wagonjwa kulala zaidi ya wawili katika kitanda kimoja.

Aidha Dk. Stefano alisema  Hospitali kwa sasa ina mpango mkakati wa kujenga jengo la gorofa mbili ambalo litagharimu kiasi cha bilioni moja hadi mbili ili kuweza kupunguza tatizo la mrundikano wa wagonjwa katika wodi hiyo.

Alisema kuwa jengo hilo litakuwa na sehemu ya upasuaji, sehemu ya mama na mtoto na watoto wanaozaliwa wachanga “njiti” (maternity complex).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM, Tawi la chuo cha kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), Mrisho Kitunga, alisema kama wasomi wameguswa na tatizo lililoko katika wodi ya mama na mtoto hospitalini hapo,  na kuweza kutoa mashuka kumi ya kujifunika pamoja na vitu mbalimbali, vyenye thamani ya shilingi laki tatu.

Naye katibu wa UWT tawi la SEKOMU, Zuhura Maulid,  alisema swala la huduma kwa jamii ni jukumu la kila mmoja wetu kuweza kuwasaidia watu wenye mahitaji na sio kuiachia serikali peke yake.

0 comments: