Winner Abraham-MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge ametoa onyo kwa kiwanda
cha NIDA Textile Mills Ltd, kutokana na kutititirisha maji yasiyo salama
kwa mazingira na afya ya wakazi wa eneo la kiwanda hicho.
Waziri Mahenge alitoa onyo hilo
wakati alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Kigogo Mkuyuni
jijini Dar es Salaam, baada ya kupata taarifa kuwa kiwanda hicho
kinatiririsha maji machafu yanayoathiri mazingira.
Awali kiwanda hicho kiliomba cheti
cha usafi wa mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira
(NEMC) na Waziri huyo aliombwa kutia saini cheti hicho ili kuthibitisha
usafi wa kiwanda hicho.
Hata hivyo, Wazari Dk Mahenge
alikuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya NIDA kukiuka
taratibu za usafi kwa kutiririsha maji machafu yanayowaathiri wananchi.
Waziri pamoja na timu yake akiwemo
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, alifanya ukaguzi wa kustukiza kwenye kiwanda
hicho na kukuta kikitiririsha maji yasiyo salama kwenye mto Kibangu
unaopita maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, baada ya Waziri na
timu yake kuingia kiwandani hapo, walitembelea maeneo mbalimbali ya
kiwanda hicho na baadaye aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kwenda
kujionea maji machafu yanayotoka kiwandani humo.
Kwa mshangao mkubwa, Waziri pamoja
na timu yake walikuta maji yaliyokuwa yakitiririshwa ni tofauti na yale
waliyoyashuhudia awali wakati walipokagua kabla.
“La kwanza ambalo ninataka
Watanzania walifahamu ni kwamba tunataka sana wawekezaji na Serikali
imeweka mazingira mazuri sana kuvutia wawekezaji, lakini mwekezaji mzuri
atakuwa ni yule tu anayejali mazingira” alisema Waziri Dk. Mahenge na
kuongeza:
“Ukiona kinachofanyika hapa ni
kama vile mwekezaji anajali cha kwake hajali maisha ya Watanzania….mimi
kwangu nimepewa malalamiko ofisini karibu mara nne, tulipita mara kwanza
na sasa tumeona haya, maana yake ni kama wenzetu hawa wanaidanganya
sekta ya uwekezaji”
Alisema kuwa walidhani ili wapate
ushirikiano mzuri ni lazima wajali mazingira ya mto huo hutumiwa
kupandwa mbogamboga, watoto wadogo wanavuka humo, hivyo wakipata
kemikali hizo watapata madhara makubwa sana.
“Maji tuliyoyakuta asubuhi sio
haya ambayo mmeenda kuyafungua sasa hivi, maana yake mitambo nyinyi
mnayo isipokuwa ama kwa gharama zenu mnazoogopa au umeme au nini
hamfungulii, vilevile mnaonekana hamuwajali Watanzania” alisema Waziri
Dk. Mahenge.
Alibainisha kuwa kwa mtindo huo
hawawezi kupewa cheti cha usafi wa mazingira kama hatapata uhakika
kwamba maji yataendelea kuwa mazuri kwa muda wote huku akinoesha hofu
kuwa iwapo watapewa cheti wataendelea kudanganya Watanzania.
Afisa Tawala wa kiwanda hicho
Mohamed Honelo aliahidi kuwa watafanya marekebisho na kuweka mazingira
katika hali ya usafi kwa muda wote na kuomba radhi kwa Serikali kutokana
na hali hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC
Bonaventure Baya alisema wanajipanga kuhakikisha kuwa wanaweka
utaratibu wa kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinazingatia masharti ya
usafi wa mazingira kwa muda wote.
0 comments:
Post a Comment