Kushoto
ni kamanda wa UVCCM Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Ibrahim Sanga, akiwa
na Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Mbozi, Warren Kaminyoge.
KUNA msemo unatumika na watu wa nyikani kuwa, mtu ambaye
haonekani kwenye shamba la karanga, hawezi kuonekana kwenye shamba la Mpunga.
Julai 6, mwaka huu, ilikuwa ni siku ya historia kwa wananchi
wa mkoa wa Mbeya.
Historia hiyo ilijikita katika tukio la kuapishwa
makamanda wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi. (UVCCM).
Tukio hilo lilifanyika katika uwanja wa CCM Ilomba,
Jijini Mbeya. Mgeni rasmi alikuwa ni mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa, Jerry
Silaa, ambaye pia ni Meya wa manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.
UVCCM imeutambua msemo wa watu wa nyikani. Sasa
wamesikia. Wameona. Wamegusa na kunusa.
Wameanza kuonekana kwenye shamba la karanga ili baadae
waonekana kwenye shamba la Mpunga.
Makamanda walioapishwa siku hiyo walikuwa ni Kamanda wa
UVCCM Mkoa wa Mbeya, Yona Sonelo, Kamanda Wilaya ya Mbozi, Ibrahim Sanga,
kamanda Wilaya ya Chunya, Philipo Mulugo, kamanda wa Wilaya ya Mbeya Vijijini,
Oran Njeza na kamanda wa Wilaya ya Mbeya Mjini, Tonebu Chaula.
Ambao hawakufika ni kamanda wa Ileje, John Cheyo, kamanda
wa wilaya ya Rungwe, Richard Kasesela, wilaya ya Momba, Twaha Kilabeba, Mbarali,
Ibrahim Mwakabwanga na Kyela Elius Asangalwisye.
Baada ya uapishwaji wa makamanda hao, ulifanyika mkutano
wa hadhara katika viwanja hivyo.
Kabla ya kuapishwa makamnada hao, kulitanguliwa na Baraza
kuu la mkoa Julai 5, mwaka huu, ambalo mgeni rasmi alikuwa ni Mwenyekiti wa CCM
mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi.
Katibu wa siasa na uenezi wa CCM, mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi,
anasema tatizo kubwa la baadhi ya vijana, wanatumika vibaya na wagombea na
kukisemea chama bila utaratibu.
“Ni kipindi kigumu sana kwenu, wakati wetu akina Guninita
waliwahi kufutwa uongozi kutokana na tabia zinazofanana na vijana wa leo.
Mnatoa matamko bila hata vikao vya chama kutoa maamuzi” anasema Madodi.
Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Mbeya
kutoka wilaya ya Momba Mbeya, Hassan Nyalile, anasema, anaunga mkono kauli ya
Madodi na kusema kuwa kauli aliyoitoa ni ya kiungozi na kwamba Makonda
anatakiwa kujirekebisha na kurudi kwenye majukumu yake.
“Makonda anatakiwa atafsiri vema kauli ya Madodi na
kurejea kwenye misingi ya kanuni ili aweze kufanya vema kazi za jumuiya yake ya
watoto badala ya kila wakati kuinuka na kutoa matamko ambayo yanaashiria yupo
na kiongozi mmoja mfukoni kutafuta nafasi ya Rais mwaka 2015”
Kwa upande wake, Paul Makonda ambaye alikuwepo kwenye
Baraza hilo, ndiye aliyeanza kueleza kuwa vijana wapo ndani ya mifuko ya
wanasiasa wakubwa, ndiyo maana inafikia mahala chama hakiwaamini.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, anasema
vijana wangoje chama kitoe maamuzi kwanza ya mgombea nafasi ya Urais ndipo
wamuunge mkono, badala ya kugawanyika kwa sasa.
Katibu wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Said Yasin, anasema umoja
ndiyo kila kitu katika kufanikisha ushindi wa chaguzi zijazo, yaani uchaguzi wa
serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2015.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza hilo, ambaye pia ni
Naibu Waziri wa Kilimo chakula na ushirika, Godfrey Zambi, anapongeza kamati ya
utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Mbeya, kwa kuendeleza kudumisha muungano kwa
kuwaalika viongozi wengine wa umoja huo kutoka mikoa mingine ya Tanzania Bara
na visiwani.
“Si vibaya ili kuendelea kudumisha muungano kuendelea
kuoleana. Nawaagiza makabitu wote kuacha tabia ya kutumia magari haya katika
kazi zao binafsi kama kwenda harusini,kanisani,sokoni ili hali kuna shughuli za
chama,vijana iwapo mtanyimwa gari na katibu yeyote kwa shughuli ya chama
nipigieni simu mimi moja kwa moja,”anasosoyiza Zambi ambaye pia ni Mbunge wa
Jimbo la Mbozi Mashariki.
Leo sauti ya nyikani haitajadili suala la Baraza hilo
wala Mkutano wa hadhara, lakini baadhi ya vijana wanaelezea kuhusu taasisi yao
hiyo.
Sauti ya Katibu wa UVCCM wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya,
George Silindu, inasema kuwa, CCM ina jambo la kujifunza kutokana na mkutano
huo wa Jumuiya yake.
Anasema ukubwa wa mkutano huo na uwingi wa watu
waliojitokeza, ni funzo kwa chama, kwa madai kuwa ushirikishwaji wa uandaaji
mikutano ni jambo jema.
Anafafanua kuwa baadhi ya mikutano ya CCM haina mwitikio
kutokana na ukiritimba wa mgawanyo wa kazi za uandaaji wa mikutano hasa zile
zinazohusu fedha.
“Katika mkutano wetu vijana kulikuwa na vyombo vyote vya
habari, kamati ya utekelezaji ilishirikisha wajumbe mbalimbali, wakiwemo
watendaji na wenyeviti,katika maandalizi na ndiyo maana mkutano ulifana kuliko
hata wa miaka 37 ya CCM Taifa” anasikika Silindu.
Anaelezea mikakati ya wilaya yake kuwa baada ya kumpata
kamanda wao wa vijana, wana mikakati ya kuhakikisha vijana wa wilaya hiyo
wanakuwa nuru kwa chama na jamii ya watanzania.
Anasema, vijana wengi waliopitia katika tanuru la UVCCM
na kuteuliwa katika ngazi za chama na serikali, hawapati shida katika kuongoza,
tofauti na wale ambao hawajapitia katika jumuiya hiyo.
Kamanda wa UVCCM wilaya ya Mbozi, Ibrahim M. Sanga, anapaza
sauti yake kuwa, licha ya yeye kutokuwa mwanasiasa wa majukwaani, anawapenda vijana.
Anasema, vijana wakipata ajira chama hicho kitakuwa
salama.
Anaeleza mikakati ya kuwainua vijana kiuchumi kuwa ni
kuunganisha nguvu na mawazo ya vijana na wadau wengine ndani na nje ya wilaya
ya Mbozi, kutengeneza mradi ambao utawapatia vijana ajira.
“Tutakuwa wilaya ya mfano kwa vijana wa chama mkoani
Mbeya, kupata ajira kupitia mradi tutakaoutengeneza, na hiyo itakuwa chachu ya
vijana kukipenda chama na nchi yao’’ anasema Kamanda huyo wa vijana wa wilaya
ya Mbozi.
“Utakuta wamekwenda kukitumikia chama na wanarudi bila
chochote kwa ajili ya maisha yao ya kila siku, ndiyo maana wanahamia vyama
vingine na kuishi kwa matumaini kuwa huenda kuna siku vyama hivyo vitapata
madaraka na wao wakapata chochote’’ anasema Ibrahim Sanga.
UVCCM ni tanuru la uongozi wa serikali na CCM.
Pamoja na ukweli huo na chama hicho kinavyoamini, vijana
hao wanapaswa kupata mafunzo kadhaa.
Chama hicho kione umuhimu wa dhahabu hii ya vijana ambao
wapo kwenye tanuru la uongozi, kupatiwa mafunzo ili wajitambue.
Mafunzo ambayo wanapaswa vijana wa UVCCM, wajifunze ni
maadili na nafasi ya vijana katika mapambano ya rushwa, nadharia ya chaguzi za
dola katika mfumo wa vyama vingi na uhusiano kati ya CCM, UVCCM na serikali.
Mada zingine ziwe ni zile zinazolenga umuhimu wa matumizi
ya vyombo vya habari na sanaa katika chaguzi, ujasiri na maarifa ya uhai wa
UVCCM, mawasiliano na uandishi wa utunzaji wa kumbukumbu.
NA GORDON KALULUNGA
Mwandishi wa makala 0754 440749
kalulunga2006@gmail.com













0 comments:
Post a Comment