Tuesday, 20 May 2014

Wachimbaji wadogo wapewa mtaji na leseni za uchimbaji


Na Nathaniel Limu, Ikungi
KAMPUNI ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Shanta Mining Ltd imetoa leseni tatu na mtaji wa shilingi milioni 40 kwa kikundi cha wachimbaji wadogo cha Aminika cha kijiji cha Mang’onyi Wilayani Ikungi, Mkoani Singida.
Kikundi hicho Aminika Gold Mine Co- Operative Society Ltd Mang’onyi, kimekabidhiwa leseni hizo hivi karibuni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stepheni Maselle kwenye kijiji cha Sambaru.
Akikabidhi leseni hizo Naibu Waziri Maselle amewataka wanakikundi kujipanga vizuri katika kuanza kufanya kazi ya uchimbaji dhahabu ili kujikwamua kimaendeleo.
Aidha amesema ni matarajio yake kuona kuwa kikundi hicho kinakuwa na maendeleo na kuwa mfano wa kuigwa hapa nchini kwani tayari nguvu kazi wamepewa mtaji na Shanta.
“Ndugu zangu sijui Mungu awape nini mmepewa leseni, mmepewa mtaji na vifaa vya kuanzia kazi na hawa wenzetu wa Tan Discovery mnaoneshwa eneo ambalo tayari limefanyiwa utafiti, sasa kazi kwenu.” Amesema Maselle huku akishangiliwa na wananchi.
Aidha aliwataka wanakikundi hao kutumia kama SACCOS katika kukopa sehemu mbalimbali za kifedha kwa manufaa yetu na kizazi cha baadae.
Hata hivyo Naibu Waziri, Maselle amesema ni dhamira ya serikali kuendeleza wachimbaji wadogo hapa nchini kwa kuwapatia mafunzo na namna bora ya uchimbaji pics masele
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Maselle akimkabidhi Katibu wa Kikundi cha Aminika Ltd cha kijiji cha Mang’onyi Wilayani Ikungi, Hamis Kingi,moja ya leseni tatu za uchimbaji wa madini ya dhahabu zilizotolewa na Kampuni ya Shanta Mining Ltd, katika hafla fupi za makabidhiano iliyofanyika Kijiji cha Sambaru.
madini.
Katika risala ya wanakikundi cha Aminika iliyosomwa na Katibu wake, Hamis Kingi amesema kikundi hicho ni muungano wa vikundi vitano kutoka vijiji   vitatu vitakavyoathirika na Mgodi wa Kampuni ya Shanta Mining vyenye jumla ya wanachama 218.
Kingi alivitaja vikundi hivyo kuwa ni Elimika Sambaru,Amani Sambaru, Amka Sambaru, Aminifu Mang’onyi na Muungano Mlumbi ambavyo kwa pamoja vimeungana   na kuwa kikundi kimoja kinachojulikana kwa jina la Aminika
Aidha alitanabaisha kwamba vikundi baada ya maelekezo hayo   ya Serikali wachimbaji waliendelea kujiunga pamoja na kuunda kikundi kilichofuata utaratibu wa kisheria wa kusajiliwa na kupata usajili namba, SIR624 Kikundi cha Aminika Gold Mine Co – Operative Society Ltd – Mang’onyi hatimaye wamekabidhiwa   rasmi na Serikali.
“Mh,Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwa kuwa kikundi kiko Kisheria tunaomba Serikali kupitia Wizara yako ya Nishati na Madini Makubaliano yetu kati ya Kampuni na Kikundi cha Aminika yaweze kutekelezeka kwa muda mwafaka, kwani wanakikundi wanahitaji kufanya kazi ili kujikwamua kiuchumi.”Alifafanua Kingi.
pics 2 masele
Naibu Waziri wa Nishati na madini Steven Maselle akizungumza na wananchi wa kijiji cha Samabru Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida wakati wa makabidhiano ya leseni tatu kwa wanakikundi cha Aminika Ltd juzi.Picha na Nathaniel Limu.
“Pia tunakushukuru wewe binafsi kwa juhudi zako kubwa kuwatetea wachimbaji wadogo kwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini.” Amesema.

0 comments: