Saturday 24 October 2015

Nani kukatwa Old Trafford wikiendi hii Angalia tathimini ya mechi ya leo man u na man city

MANCHESTER, ENGLAND

VINARA wa Ligi Kuu ya England, Manchester City, Jumapili hii watawatembelea mahasimu wao wa mji mmoja Manchester United kwenye mchezo wa mzunguko wa 10 wa Ligi Kuu ya England (EPL) utakaopigwa ndani ya dimba la Old Trafford. 

Timu hizi zinatenganishwa kwa tofauti ya alama moja pekee kwenye msimamo wa EPL, hivyo mchezo baina yao utakuwa wa kusisimua kupita kiasi.

Itakumbukwa mara ya mwisho timu hizi zilipokutana Aprili 12 mwaka huu ndani ya Old Trafford, Man United waliweza kutoka kifua mbele baada ya kuwatandika mahasimu wao mabao 4-2. 

Kabla ya mchezo huo, Man United walikutana na vipigo vinne mfululizo kila walipocheza na wapinzani wao hao kutoka jijini Manchester, Man City.

Man United bado hawajapoteza mchezo wowote wa EPL kwenye dimba lao la nyumbani Old Trafford msimu huu, ambako wameshinda michezo mitatu dhidi ya Tottenham, Liverpool na Sunderland na kutoa sare mmoja dhidi ya Newcastle United. 

Man City ambao wamekusanya jumla ya alama 21 mpaka sasa, wameshinda michezo mitatu ya EPL dhidi West Bromwich Albion, Everton na Crystal Palace kati ya michezo minne ya ugenini. 

Mchezo pekee wa ugenini waliopoteza ni dhidi ya Tottenham Hotspurs, kipigo cha mabao 4-1.
Pengine kipigo hicho walichokipata kwenye dimba la White Hart Lane mwezi mmoja uliopita, kinawapa tahadhari kuelekea kwenye dimba la Old Trafford.

Hata hivyo, kitakwimu Man City ni timu tishio mno kwenye EPL msimu huu. Vinara hao wa EPL ndiyo timu inayoongoza kwa kupachika mabao mengi mpaka sasa, ikiwa na jumla ya mabao 24. 

Man United wapo nyuma kwenye idadi ya mabao ya kufunga, wakiwa wametikisa nyavu za timu pinzani mara 15 pekee, ambayo ni machache ukilinganisha hata na idadi ya mabao ya Arsenal, West Ham na Leicester City.

Hii inaonyesha kuwa safu ya ushambuliaji ya Manchester United haiyakaribii hata kidogo makali ya safu ya ushambuliaji ya Manchester City. 

Walinzi wa Man United watatakiwa kuwa macho dakika zote za mchezo watakazokuwa wakipambana kuwadhibiti washambuliaji wa Man City wasisababishe madhara.

Vilevile takwimu za wastani wa mashuti kwa mchezo mmoja wa EPL zinaonyesha umahiri wa Man City kwenye suala la ushambuliaji. 

Wababe hao wa Etihad wanaongoza kwa wastani wa mashuti kwa mchezo mmoja wakiwa na wastani wa mashuti 20 kwa mchezo. 

Hii ina maana kuwa, watapiga takribani mashuti 20 ikiwa watakuwa kwenye ubora wao wa siku zote.

Man United wao wana wastani wa mashuti 11 pekee kwa mchezo mmoja. Hiki ni kielelezo kingine cha udhaifu wao kwenye upande wa ushambuliaji wanapolinganishwa na mahasimu wao Man City.

Kwa upande wa vikosi, Manchester United wanao majeruhi watatu ambao ni Ashley Young, Luke Shaw na Patrick McNair ambao hawatjumuishwa kwenye mchezo huu. 

Hata hivyo, City ndio wanaokabiliwa na mapengo ya wachezaji muhimu zaidi wakiwamo Sergio Aguero na David Silva wanaosumbuliwa na majeraha. 

Majeruhi wao wengine ni Fabian Delph na Gael Clichy.

Nyota wa kuchungwa kwa upande wa Man United ni Anthony Martial ambaye kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hivi karibuni dhidi ya CSKA Moscow, alifunga bao lake la tano tangu alipojiunga na Manchester United. 

Kwa upande wa Manchester City, Kevin De Bruyne ndiye nyota anayeng’ara zaidi kwa sasa, akiwa amefunga mabao manne na kutengeneza mengine matatu tangu alipojiunga na timu hiyo.

Nani kulia, nani kucheka? Ni suala la kusubiri, kwani mpira ni dakika 90.

0 comments: